• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:03 AM
Uswisi wadengua vigogo Ufaransa na kujikatia tiketi ya kuvaana na Uhispania kwenye robo-fainali za Euro

Uswisi wadengua vigogo Ufaransa na kujikatia tiketi ya kuvaana na Uhispania kwenye robo-fainali za Euro

Na MASHIRIKA

KYLIAN Mbappe alipoteza mkwaju muhimu katika mchuano ulioshuhudia Uswisi wakibandua mabingwa wa dunia Ufaransa kwenye hatua ya 16-bora ya Euro kupitia penalti mnamo Jumatatu usiku.

Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa Uswisi ya kocha Vladimir Petkovic kuvuna katika hatua ya mwondoano kwenye mapambano ya haiba kubwa tangu 1938.

Uswisi walikuwa pua na mdomo kudenguliwa kwenye kampeni hizo katika kipindi cha kawaida cha dakika 90. Hata hivyo, walisawazisha mambo kuwa 3-3 katika dakika za mwisho na kulazimisha mshindi wa mchuano uliowakutanisha na Ufaransa kuamuliwa kupitia penalti.

Haris Seferovic aliwaweka Uswisi kifua mbele katika dakika ya 51 na akapoteza ambayo ingewapa uongozi wa 2-0 kufikia dakika ya 55. Hata hivyo, Ufaransa walirejea mchezoni kupitia kwa Karim Benzema aliyesawazisha katika dakika ya 57 na kukiweka kikosi chao uongozini dakika mbili baadaye.

Kiungo matata wa Manchester United, Paul Pogba alifanya mambo kuwa 3-1 katika dakika ya 75. Japo dalili zote ziliashiria kwamba Ufaransa wangeibuka washindi kufikia hapo, Uswisi hawakufa moyo. Walijituma maradufu mwishoni mwa kipindi cha pili na wakafunga mabao mawili ya haraka kupitia Seferovic na Mario Gavranovic katika dakika za 81 na 90 mtawalia.

Mbappe alipoteza nafasi nyingi za kufungia Ufaransa bao la ushindi katika muda wa ziada huku Olivier Giroud akishuhudia kombora lake katika dakika ya 119 likidhibitiwa vilivyo na kipa wa Uswisi, Yann Sommer.

Mbappe ambaye ni mchezaji wa Paris Saint-Germain (PSG) nchini Ufaransa, ndiye wa pekee aliyeshindwa kufunga penalti baada ya mkwaju wake kupanguliwa na Sommer na mechi hiyo kukamilika kwa 5-4.

Uswisi sasa watavaana na Uhispania ambao pia waliangusha Croatia kwa mabao 5-3 katika muda wa ziada. Robo-fainali hiyo itachezewa jijini St Petersburg, Urusi mnamo Julai 2, 2021.

Ushindi uliosajiliwa na Uswisi dhidi ya Ufaransa ndiyo matokeo ya kuduwaza zaidi ambayo yameshuhudiwa katika kipute cha Euro kufikia sasa mwaka huu. Hii ni kwa sababu Ufaransa ni miongoni mwa vikosi vilivyokuwa vikipigiwa upatu wa kunyanyua ufalme wa kivumbi hicho chini ya kocha Didier Deschamps.

Mara ya mwisho kwa Uswisi kunogesha robo-fainali za kipute chochote cha haiba kubwa katika ulingo wa soka ni 1954 walipokuwa wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia.

Hadi wakati huo, hawakuwa wamewahi kusonga mbele zaidi ya hatua ya mwondoano tangu 1938 kwenye Kombe la Dunia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Seli kwa kusimika bendera ya Somalia

Uhispania waingia robo-fainali za Euro baada ya kuangusha...