• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Seneta wa Garissa Yusuf Haji afariki

Seneta wa Garissa Yusuf Haji afariki

Na SAMMY WAWERU

SENETA wa Garissa, Bw Yusuf Haji amefariki mapema Jumatatu, imetangaza familia yake.

Bw Haji na ambaye ni babake Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma ((DPP) Noordin Haji, ameaga dunia wakati akipokea matibabu katika Hospitali ya Aga Khan – Nairobi.

Bw Haji amekuwa akiugua kwa muda wa miezi kadhaa, na mwaka uliopita, 2020 alisafirishwa Uturuki kwa matibabu zaidi.

Alirejeshwa nchini majuzi. Akiongoza taifa katika kumuomboleza, Rais Uhuru Kenyatta ametaja kifo cha Seneta Haji kama pigo kwa nchi.

“Ni pigo kwa taifa kumpoteza, alikuwa kiongozi mkakamavu na nguzo kuu kufanikisha Mpango wa BBI,” Rais Kenyatta ameeleza kupitia taarifa.

“Kenya imepoteza kiongozi mzalendo na mwenye maono, kiongozi mnyenyekevu. Tunamshukuru kwa utendakazi bora aliofanyia nchi hii, jitihada zake katika BBI,” kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga amemuomboleza.

Kulingana na familia yake, marehemu atazikwa saa kumi alasiri hii leo, katika makaburi ya Dini la Kiislamu ya Lang’ata, jijini Nairobi.

Aidha, amefariki akiwa na umri wa miaka 80.

Baada ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Raila Odinga kuzika tofauti zao za kisiasa Machi 2018 kupitia salamu za maridhiano maarufu kama Handisheki, Seneta huyo aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa jopokazi la kuandaa Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

You can share this post!

TANZIA: Seneta Haji afariki

BBI yaunganisha vigogo wa Mulembe