• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Seneti kuwachukulia hatua wanaochelewesha miradi ya kaunti licha ya kubugia mamilioni

Seneti kuwachukulia hatua wanaochelewesha miradi ya kaunti licha ya kubugia mamilioni

NA MARY WANGARI

SENETI imependekeza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mashirika na wafanyabiashara wanaochelewesha miradi ya kaunti licha ya kupokea mamilioni ya pesa za walipaushuru kama malipo.

Katika kikao kilichoandaliwa Jumanne, Kamati ya Seneti inayosimamia Hesabu za Umma ilielezwa kuwa baadhi ya kaunti zina miradi iliyoanzishwa tangu 2014 na ingali haijakamilika hadi sasa hali inayolemaza maendeleo katika kaunti.

Kaunti za Homabay na Nandi zilitajwa kama miongoni mwa kaunti zilizoathirika zaidi huku zikiwa na miradi iliyokwama kwa karibu miaka tisa licha ya rekodi kuonyesha malipo ya bidhaa husika.

Gavana wa Kaunti ya Homabay, Gladys Wanga alikabiliwa na wakati mgumu kufafanua ni kwa nini miradi ya Kiwanda cha Mahindi cha Kigoto na cha Malisho ya Mifugo bado haijakamilika tangu ilipoanzishwa 2014.

Mkuu huyo wa kaunti alikuwa amefika mbele ya Kamati hiyo kujibu maswali kuhusu usimamizi wa fedha katika kaunti hiyo.

“Kitita cha Sh16 milioni kililipwa mnamo 2014 wakati mradi huo wenye thamani ya Sh42milioni ulipoanzishwa. Miaka mitano baadaye, hakuna mashine zilizokuwa zimewasilishwa licha ya malipo kutolewa,” ilisema ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Kulingana na Gavana Wanga, mashine hizo ziliwasilishwa mnamo Novemba 2021, lakini zingali kwenye kontena na hazijaanza kutumika.

“Kwa sababu mitambo hiyo ilinunuliwa mnamo na serikali ya kaunti iliyokuwapo 2014, hatuna hakika ikiwa ingali mwafaka kimiundo na kiteknolojia. Tulisema hatutalipa hata senti hadi tutakapokuwa na hakika kuwa mashine hiyo bado inaweza kutumika,” alisema Gavana Wanga.

Aidha, Gavana Wanga alionekana kutatizika kufafanua ni kwa nini ujenzi wa ua kwenye Kiwanda cha Mahindi cha Kigoto uligharimu zaidi ya Sh3 millioni.

Mradi huo bado haujaanza kufanya kazi zaidi ya miaka saba tangu ullipoanzishwa, Seneti ilielezwa.

“Tulipozuru kiwanda hicho, hakikuwa na ua wowote. Ulikuwa umeharibiwa na ilitulazimu kuanza upya. Kando na Sh1.8 zilizokuwa zimelipwa awali, ilitulazimu kutumia Sh2.01 milioni zaidi kujenga ua mpya,” alieleza.

Usimamizi wa Kaunti hiyo, hususan serikali zilizotangulia zimeshutumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha za umma huku Seneti ikitaka wahusika wote wakabiliwe kisheria.

“Hatuwezi kupuuza kuwa kuna mtu aliyeidhinisha asilimia 89 ya mradi huo kama ulio kamilika ilhali hakutimiza wajibu wake huku mradi ukikamilika baada ya miaka saba. Huu ni ubadhirifu wa pesa za umma. Ni sharti tuchukue hatua dhidi ya wanaokaa na pesa za kaunti kwa miaka bila kufanya chochote,” alisema Seneta John Methu, ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya Seneti kuhusu Ardhi, Mazingira na Raslimali Asilia.

Wakati huo vilevile, Seneti ilielezea wasiwasi wake kuhusu tabia ya magavana kuingilia miradi maarufu ya serikali kuu huku wakitelekeza miradi ya mashinani wanayosimamia.

“Serikali za kaunti zinajishughulisha na miradi maarufu bila kuzingatia Kanuni ya Nne kuhusu Ugavi wa Majukumu Kati ya Serikali Kuu na Serikali za Kaunti. Kaunti zimejitwika jukumu la kupatia wanafunzi basari kwa sababu ni maarufu,”alisema Seneta wa Busia Okiya Omtatah.

“Bado sijaona Kaunti yoyote inayofanya kazi nzuri kuhusu shule za chekechea ilhali kuna mengi mno yanayohitajika. Kutoa basari kunaweza kuwa jambo maarufu lakini si halali.”

  • Tags

You can share this post!

Nyota ya Mudavadi yang’aa serikalini

Upinzani nchini Nigeria wapinga matokeo ya urais

T L