• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Upinzani nchini Nigeria wapinga matokeo ya urais

Upinzani nchini Nigeria wapinga matokeo ya urais

NA MASHIRIKA

ABUJA, NIGERIA

VYAMA vya upinzani nchini Nigeria vikiongozwa na chama cha Peoples Democratic Party (PDP) vimepinga matokeo ya urais yalitotangazwa na Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (INEC) vikidai uchaguzi huo ulitawaliwa na wizi wa kura.

Vyama hivyo vilidai kwamba njama ilipangwa ya kumwibia kura mgombea wa urais Bola Tinubu.

Hii ni baada ya tume hiyo kumtangaza Tinubu, mwanasiasa mkongwe mwenye umri wa miaka 70 kuwa mshindi wa kiti hicho.

Kwa mujibu wa matangazo hayo, Tinubu alipata kura 8.8 milioni (asilimia 36) huku mpinzani wake mkuu Atiku Abubakar akipata asilimia 29 naye Peter Obi wa chama cha Labour akipata asilimia 25.

“Hatutambui ushindi wa Tinubu. Matokeo ya urais hayakuwekwa wazi kwenye tovuti ya tume hiyo. Uchaguzi huo pia ulitawaliwa na changamoto kadha ikiwemo vurugu. Tatizo kuu lilitokea katika kituo cha kujumuisha kura. Hii inatuonyesha kwamba kulikuwa na njama ya kuiba kura,” akaeleza Dino Melaye ambaye ni Wakala wa Atiku Abubakar.

Kabla ya matokeo kutangazwa, Abubakar, aliirai tume hiyo kuweka matokeo kwenye tovuti yake mara moja baada ya kuyapokea. Aliwalaumu baadhi ya magavana wa majimbo kwa kujaribu kubadilisha matokeo hayo.

“Itakuwa vibaya ikiwa yeyote atajaribu kubadilisha uamuzi wa raia kwa kubadilisha matokeo ya uchaguzi,” alisema kwenye taarifa.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Mahmood Yakubu, alijitetea akisema kwamba uchaguzi huo ulikuwa wazi.

Uchaguzi huo uliofanyika Februari 25 umekumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo vurugu.

Hii ni baada ya tume hiyo kuchelewa kutangaza matokeo kinyume na ilivyoahidi kabla ya uchaguzi.

Hatua ya tume hiyo kuchelewa kuweka matokeo hayo kwenye tovuti yake Jumanne ilizua hofu ya wizi wa kura kutokea.

Madai hayo yamekuwa yakitolewa kwenye chaguzi kadhaa ambazo zimefanyika nchini humo hapo awali.

Jumuiya ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) pia iliponda tume hiyo ikiishutumu kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake.

Jumuiya hiyo ilianisha matatizo mbalimbali yaliyokumba uchaguzi huo ikisema kwamba imechangia katika uwepo wa wizi wa kura.

“Baadhi ya vituo vililazimishwa kusimamisha upigaji kura kwa sababu ya vurugu. Wasimamizi wa uchaguzi pia walilazimika kutembea katika vituo mbalimbali kukusanya matokeo. Hii ni kwa sababu tume hiyo ilishindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu,” akasema Ernest Koroma, Msimamizi wa ECOWAS.

Tinubu ni mmoja wa wanasiasa tajiri zaidi Nigeria, na aliahidi kufufua uchumi wa nchi hiyo ambao umezorota.
Tinubu alizoa kura kadhaa katika baadhi ya majimbo, jambo lililomuweka mstari wa mbele.

Uchaguzi huo ulikumbwa na ucheleweshaji na madai ya majaribio ya wizi wa kura.

Rais huyo mpya anatarajiwa kupambana na masuala ya kuzorota kwa uchumi na ukosefu wa usalama.

  • Tags

You can share this post!

Seneti kuwachukulia hatua wanaochelewesha miradi ya kaunti...

TAHARIRI: Serikali yafaa imalize wizi wa chakula cha msaada

T L