• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Serikali yazima wanahabari wasifichue uzembe wake katika shule

Serikali yazima wanahabari wasifichue uzembe wake katika shule

Na WAANDISHI WETU

WANAHABARI Jumatano walijipata matatani baada ya mawaziri George Magoha (Elimu) na Dkt Fred Matiang’i (Usalama) kuwazuia kuandamana nao kwenye ziara zao shuleni, kwa kisingizio cha “kuwapotosha Wakenya” kuhusu hali ilivyo katika shule nchini.

Agizo hilo pia lilitolewa na Naibu Waziri wa Elimu Zack Kinuthia, aliyesema kuwa lazima wanahabari wapate kibali kutoka kwa wizara hiyo kuingia katika shule yoyote ili kupiga picha.

Akihutubia wanahabari jijini Nairobi jana, Prof Magoha alisema agizo hilo linalenga kuwapa wanafunzi, hasa watahiniwa wa Darasa la Nane na Kidato cha Nne muda wa kutosha kuendelea na masomo yao bila usumbufu wowote.

Alisema hilo pia linatokana na hali kuwa huu ni Muhula wa Tatu kwao.

“Nawaomba kutofika shuleni kwani nina kikosi ambacho kina uwezo kuangazia hali ilivyo kwenye taasisi hizo. Sababu kuu ni kuwa mtihani ni suala lenye uzito sana. Hakuna mgeni ambaye ataruhusiwa kuingia humo,” akasema.

Hata hivyo, aliongeza kuwa wizara hiyo haifichi lolote kwa wananchi.

Prof Magoha alisema hatua hiyo inafuatia agizo lililotolewa na Rais Uhuru Kenyatta hapo Jumapili, ambapo alisema watu wasiohusiana na mahitaji ya wanafunzi hawapaswi kuruhusiwa kuingia shuleni.

Wanahabari katika Kaunti ya Tharaka Nithi pia walijipata kwenye njiapanda, baada ya Dkt Matiang’i kuwazuia kuandamana naye alipozuru shule kadhaa kuangazia jinsi zinavyoendeleza masomo.

Waziri alisema ana kikosi cha mawasiliano ambacho kitaangazia taswira kamili kuhusu hali ilivyo shuleni.

Wanahabari walioandamana naye walizuiwa kupiga picha katika shule alikozuru.

Baraza la Vyombo vya Habari (MCK) limekuwa likisisitiza kuwa ni ukiukaji wa haki za wanahabari kwa maafisa wa serikali kuwazuia kuangazia hali ilivyo.

“Ni haki ya wanahabari kuangazia hali ilivyo nchini ili kuufahamisha umma kuhusu hali ilivyo bila kuficha lolote,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa baraza hilo, Bw David Omwoyo kwenye kikao cha awali.

Wakati huo huo, shule sita katika Msitu wa Boni zimeendelea kubakia zimefungwa licha ya wanafunzi kurejelea masomo yao Jumatatu.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kwamba shule za msingi za Bodhai, Milimani, Basuba, Mangai, Mararani na Kiangwe zilizo ndani ya msitu huo hazikuwa zimefunguliwa kufikia Jumatano baada ya walimu kukosa kufika shuleni.

Hali hiyo imewafanya zaidi ya wanafunzi 400 wa shule hizo kusalia nyumbani na wazazi wao huku wenzao wakiendelea na masomo yao kama kawaida.

Kwenye mahojiano, wazazi wengi walieleza wasiwasi wao kuhusu hali ilivyo, ikizingatiwa shule nyingi zimekuwa zikifungwa mara kwa mara kutokana na mashambulio ya kundi la wapiganaji wa al-Shabaab.

Katika Kaunti ya Uasin Gishu, hali ya umaskini imefanya idadi kubwa ya wanafunzi kutoka Shule ya Msingi ya Langas mjini Eldoret kukosa barakoa.

Shule hiyo ni miongoni mwa zile zenye idadi kubwa ya wanafunzi eneo hilo.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bw Chrispin Owako alisema hali hiyo imewafanya baadhi ya wanafunzi kuombana barakoa.

Mtindo wa wanafunzi kuombana ama kubadilishana barakoa umezua malumbano ya aina yake kwenye mitandao ya kijamii.

Ripoti za Wanderi Kamau, Faith Nyamai, Alex Njeru, Kalume Kazungu, Titus Omide na Sammy Waweru

You can share this post!

BI TAIFA JANUARI 7, 2021

TAHARIRI: Serikali inatuficha nini huko shuleni?