• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Sheng si lugha ya mahakamani, mtuhumiwa aonywa

Sheng si lugha ya mahakamani, mtuhumiwa aonywa

Na RICHARD MUNGUTI

SHAHIDI katika kesi ya wizi wa watoto katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki iliyoko mtaani Umoja Nairobi Jumatatu alitahadharishwa dhidi ya kuzugumza lugha ya Sheng akitoa ushahidi.

Bw Morris Nguyo Muli, ambaye ni mhandisi wa kutengeneza magari alitahadharishwa alipoanza kusema alisikia “kilio cha mtoto aliyekuwa ametupwa katika kibanda cha kuuza mboga na alikuwa “jinni” iliyokuwa ikilia kama paka.”

Bw Muli aliyekuwa anatoa ushahidi katika kesi dhidi ya wafanyakazi wawili wa hospitali hiyo ya Mama Lucy Selina Adunda Awuor na Makalla Fred Leparan ya wizi wa watoto alisema “alipata mshtuko alipomsikia mtoto akitoa mlio kama wa paka”

Bw Muli aliyekuwa ameandamana na wakili rafikiye Bw Brian Kimeu Muia wakitoka kubugia pombe katika kilabu kimoja kilicho eneo la Sinai,Viwandani.

Shahidi huyo alisema walikuwa wanaelekea nyumbani Mei 4,2020 walipofika kwenye vibanda vilivyoko barabara ya Outering walisikia mtoto akilia lakini wakasikia kama ni “ paka”

“Nilimweleza Bw Muia..mmoja wa bogi yangu kwamba hiyo ni Jinni..sio mtoto..unajua watu wanayafuga kuimarisha biashara zao,” alisema Bw Muli alipoongozwa kutoa ushahidi na kiongozi wa mashtaka Bi Evalyne Onunga.

Shahidi huyo aliulizwa na hakimu mwandmizi Bi Esther Kimilu wa mahakama ya Milimani Nairobi, “bogi ni nini.”

Shahidi huyo aliyekuwa amevalia suti na fulana alijaribu kueleza lakini akasababisha kicheko zake kwa kuzugumza sheng ya ndani.

“Utawacha hiyo ya lugha ya Eastlands..Hii ni mahakama..lugha rasmi hapa ni kiingereza na Kiswahili,” hakimu alimkumbusha shahidi.

Aliendelea kusema walisongea karibu ya kile kibanda kisha wakaingia ndani.

Washtakiwa Selina Awuor na Makalla Fred Leparan. PICHA/ RICHARD MUNGUTI

Akasema , “ Tulimpata mtoto amewekwa ndani ya katoni amefungwa shuka ya Wamasai.Kitovu chake kilikuwa kimefengwa na Pegi. Kitovu kilikuwa majimaji na mwili wa mtoto ulikuwa na makovu.”

Shahidi huyo alieleza jinsi walienda kwa Mzee wa Kijiji kumpelekea mtoto.

“Mzee wa kijiji alizunguka manyumba akimsaka mama aliyezaa na hakufanikiwa,” alisema Muli.

Hatimaye tulienda kituo cha polisi cha Savanna kuripoti.

Bw Muli alisema mtoto huyo mvulana alipewa jina la Muli la “Taji”.

Shahidi huyo alisema ,” Mtoto huyo alininyia kinyesi cheusi kabisa nikashtuka.Nilimpigia dada yangu simu ambaye ni daktari akatushauri vile tutafanya kumshughulikia mtoto.”

“Katika kituo cha polisi tulipewa barua kumpeleka mtoto hoyo hospitali ya Mama Lucy Kibaki,” alikumbuka Muli.

Shahidi huyo alisema walipofika Mama Lucy Kibaki walipokewa na Bw Leparan.

Yeye (Leparan) na Awuor walimchukua mtoto kutoka kwetu na kumpeleka katika wadi ya watoto.

Shahidi huyo aliyekuwa anaongozwa kutoa ushahidi na Bi Evalyn Onunga alisema tangu walipompeleka mtoto huyo Mama Lucy walimtembelea mara moja na hawakumwona tena.

Bw Muli alikuwa akitoa ushahidi katika kesi ambapo Selina na Makalla wameshtakiwa kuiba watoto.

Walitiwa nguvuni baada ya shirika la utangazaji la BBC kufichua kulikuwa na kashfa ya kuwaiba watoto mle hospitali na kuwauza.

Pia taarifa iliyopeperushwa ilisema muhusika mkuu alikuwa Leparan.

Lakini wakijibu maswali ya wakili Danstan Omari wakili Muia pamoja na Bw Muli walieleza korti “hawakushuhudia washtakiwa wakishiriki biashara hiyo ya kuuza watoto.”

Washtakiwa wamekana kati ya Machi na Mei 2020 waliwaiba watoto wenye umri kati ya siku sita hadi miezi miwili.

Wako nje kwa dhamana. Kesi inaendelea kusikizwa.

  • Tags

You can share this post!

Mwenyekiti wa BBI azikwa bila cheche za siasa

BBI: Madiwani wataka kikao na Uhuru, Ruto