• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Shirika la Heifer lahimiza vijana wawe mstari wa mbele kuimarisha kilimo na ufugaji

Shirika la Heifer lahimiza vijana wawe mstari wa mbele kuimarisha kilimo na ufugaji

NA SAMMY WAWERU

SHIRIKA moja lisilo la kiserikali (NGO), limezindua mipango kuhamasisha vijana kujua na kufanya shughuli za kilimo na ufugaji na kuikumbatia sekta hiyo kama mwajiri muhimu.

Mradi huo kulingana na Heifer International, pia unalenga wakulima wa mashamba madogo nchini na kuwapa vijana motisha kuendeleza zaraa.

Ukiwa unaegemea bunifu za kiteknolojia, vilevile unaazimia kusaidia sekta ya kilimo na ufugaji kukumbatia mifumo ya kidijitali.

Wadauhusika katika mtandao pana wa uzalishaji chakula nchini, wamekuwa wakiendeleza kampeni kuhamasisha sekta ya kilimo kuboreshwa kupitia teknolojia za kisasa.

Mradi wa Heifer una mipango mitatu; tuzo ya AYuTe Africa Challenge, Digital Agriculture Champions na Tractors 4 Africa Project.

Kulingana na shirika hilo, mipango hiyo inapania kutafutia vijana nafasi tele za ajira katika kilimo.

“Ni hatari kugaragaza mjadala wa kilimo, bila kuhusisha vijana,” akasema Esta Kamau, Mkurugenzi Mkuu Heifer Kenya.

Akizungumza jijini Nairobi wakati wa uzinduzi rasmi wa mipango hiyo, Esta alitangaza kufunguliwa kwa shindano la AYuTe linalolenga vijana wenye bunifu za kiteknolojia kufanikisha shughuli za kilimo.

“Droo ya AYuTe inashirikisha yeyote mwenye ubunifu katika sekta ya kilimo,” afisa huyo akadokeza.

Wanaotuma maombi wana hadi Julai 14, mwaka huu, 2022.

Mpango wa Digital Agriculture Champion, nao unalenga vijana walioko maeneo ya mashambani wenye mchango kuzalisha chakula nchini.

Tractors 4 Africa Project, Esta alisema inahusisha utoaji wa mashine za kilimo kama vile trakta na vifaa vinginevyo kwa mikopo.

Watakaonufaika hata hivyo wataanza kama maajenti wa kuuza mashine na mitambo ya kilimo, hatua ambayo itawasaidia kuwa wamiliki kupitia ulipaji wa fedha kidogo kidogo.

“Unawiana na maajenti wa M-Pesa, huduma za Benki ya Cooperative na Equity katika usambazaji pesa. Hatimaye wataweza kumiliki trekta na vifaa vingine kuendeleza shughuli za zaraa,” akafafanua.

Mwaka jana, Heifer International ilitoa ripoti iliyoonyesha vijana wanataja ukosefu fedha, umiliki wa mashamba na maarifa-ujuzi kushiriki kilimo na ufugaji kama vikwazo vinavyowazuia.

Shirika hilo aidha linahimiza wadau katika katika sekta ya umma na kibinafsi, wanaopiga jeki sekta ya kilimo na ufugaji nchini kuungana kusaidia vijana kuingilia ukulima.

Uzinduzi wa mipango ya Heifer International kuhamasisha vijana nchini kuwa katika mstari wa kilimo kupiga jeki sekta ya kilimo PICCHA | SAMMY WAWERU

Baadhi ya waliohojiwa katika utafiti wa 2021, walisema kilimo ni cha waliostaafu na wakongwe.

“Mtandao wa uzalishaji chakula ni pana, si lazima wawe shambani. Wanaweza kushiriki kutoa ushauri nasaha kufanya kilimo bora, kusafirisha mazao sokoni, kuyauza, kuongeza thamani kati ya biashara nyingi zilizoko katika sekta hii faafu,” Esta akaambia Taifa Leo majuzi.

Kulingana na Taasisi ya Unakili wa Takwimu Nchini (KNBS), sekta ya kilimo inachangia asilimia 33 katika ukuaji wa uchumi na maendeleo, GDP.

  • Tags

You can share this post!

Uhuru aongoza mkutano wa marais wa EAC kujadili mzozo wa...

CHARLES WASONGA: Ruto anahadaa, biashara ya mitumba...

T L