• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 1:57 PM
Shirika laangazia dhuluma, mahangaiko ya wasichana kipindi cha janga la Covid-19

Shirika laangazia dhuluma, mahangaiko ya wasichana kipindi cha janga la Covid-19

Na LAWRENCE ONGARO

WASICHANA wapatao 2 milioni wa umri wa kati ya miaka 12 na 16 walidhulumiwa na kupata mahangaiko ikiwemo kupata mimba katika kipindi cha janga la Covid-19.

Kulingana na shirika la utafiti la Africa Disaster Management, imebainika kuwa, Kaunti ya Kilifi ndiyo inaongoza katika msimamo huo.

Bw Peter Maina ambaye ni mkurugenzi katika shirika hilo alieleza ya kwamba idadi ya wasichana waliopata ujauzito imeongezeka kwa kiwango kikubwa nchini, jambo linalotia wasiwasi.

Alieleza kuwa shirika hilo limejitolea kuona ya kwamba wasichana hao wanahamasishwa na kupewa msaada ili kupunguza mienendo hiyo ya kupata mimba za mapema na dhuluma nyinginezo.

“Ukosefu wa fedha na familia zisizojiweza kifedha kumechangia matukio hayo yote kutendeka,” alisema Bw Maina.

Alisema ufukara ni chanzo cha wasichana wengi kujipata katika hali hiyo, huku akitaja hamasisho kama jambo muhimu kwao.

Alizidi kueleza kuwa wasichana wengi wanaotoka familia maskini hushindwa kununua sodo.

“Kutokana na hali hiyo, wanaume huwahadaa eti watawanunulia sodo halafu baadaye wanapata mimba,” alifafanua mkurugenzi huyo.

Alisema shirika hilo litafanya juhudi kuona linasambaza sodo za kisasa katika kaunti zote nchini zitakazotumika na wasichana wanaohitaji.

Aliyasema hayo eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu mnamo Jumamosi.

Alizidi kueleza kuwa katika kipindi hiki cha janga la Covid-19 wasichana wengi walipata mimba kupitia kwa jamaa zao wa karibu, jambo ambalo limezua wasiwasi katika jamii.

Wazazi nao wamepewa changamoto kuwa mstari wa mbele kuzungumza na wana wao wa kike ili wasizidi kupata mimba za mapema.

Bi Prudence Kai kutoka Kaunti ya Kilifi, aliwahimiza wazazi kuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wana wao wa kike jinsi ya kuepuka vishawishi vya wanaume kuhusu ngono.

“Wazazi wako na nafasi nzuri ya kuwahamasisha wana wao wa kike ili wasije wakaingia katika mtengo wa wanaume,” alisema Bi Kai.

Alitaka serikali iwe katika mstari wa mbele kuona ya kwamba wasichana wa umri mdogo wanalindwa kutoka kwa wanaume.

You can share this post!

JAMVI: Hofu waliohamia Tangatanga ni ‘majasusi’

JAMVI: Vizingiti vya Raila kugeuzwa kuwa mradi wa Uhuru