• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 3:09 PM
Shule ya Upili ya St Edward Nyabioto – Kisii yamulikwa kwa utepetevu mwanafunzi kupotea

Shule ya Upili ya St Edward Nyabioto – Kisii yamulikwa kwa utepetevu mwanafunzi kupotea

NA WYCLIFFE NYABERI

FAMILIA moja katika kijiji cha Geteni, Kaunti ya Nyamira inaililia serikali kuisaidia kutafuta mtoto wao baada ya kutoweka mnamo Julai 10, 2023 akiwa mikononi mwa walimu.  

Kulingana na Mzee Nicodemus Atwanga, mwanawe Reuben Ondieki, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya St Edward Nyabioto eneobunge la Bomachoge Borabu, Kisii alifukuzwa shuleni baada ya kukiri kuiba bidhaa za mwanafunzi mwenza bwenini.

Kijana Ondieki, 17, alitakiwa kurejea shuleni akiwa ameandamana na mzazi wake.

Mwanafunzi huyo hakufika kwao, sasa ikiwa ni karibu mwezi mmoja tangu apotee wasijue aliko.

Familia yake inapozidi kutaka majibu, Bw Atwanga analaumu uongozi wa shule akidai hakuarifiwa mwanawe ametumwa nyumbani.

Anaambia Taifa Leo Dijitali kwamba alifahamishwa siku iliyofuata, kwa njia ya simu.

“Nilishangaa jinsi wanaweza kutuma mtoto nyumbani bila kuarifu mzazi. Hadi kufikia sasa hatujui alikoenda,” Bw Atwanga alisema.

“Nalaumu wasimamizi wa shule kwa kutoweka kwa mwanangu. Hawakuniarifu walipokuwa wakimtuma nyumbani. Wangeniambia ningemwendea,” Bw Atwanga alisema kwa njia ya simu.

Juhudi za kumpata mwalimu mkuu wa shule hiyo azungumzie suala hilo, ziliambulia patupu kwani simu na jumbe zetu hazikuwa zimejibiwa hadi wakati wa kuchapisha taarifa hii.

Akizungumzia uchungu ambao familia yake inapitia, baba huyo wa watoto wanne alisema hajawahi kupata usingizi tangu mwanawe apotee.

“Tumetafuta kila mahali, hata kwa ndugu zetu lakini juhudi zetu zote hazijazaa matunda. Kama familia, tunavumilia kukosa usingizi usiku na imekuwa vigumu kwa baadhi ya wanafamilia yangu kula. Hakika tumetatizika,” Bw Atwanga alisema, akiskiza kutatizika.

Alisema hiyo ni kesi ya kwanza ya utovu wa nidhamu ambayo mtoto wake alihusika, japo kwa jumla alimtaja kuwa ni mtu mwenye maadili mema.

Familia imeripoti kutoweka kwake katika Kituo cha Polisi cha Kenyenya chini ya Nambari 31/14/07/2023.

Aidha, inamtaka Waziri wa Elimu Bw Ezekiel Machogu kuingilia kati shule husika itoe majibu mtoto wao alikopotelea.

Kimaumbile, mwanafunzi huyo ana rangi ya kahawia. Yeye ni mrefu na ni mwembamba.

 

 

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Mpangilio wa usafiri Lamu wasalia pale pale

Kikosi maalum kupambana na Al-Shabaab Kaskazini Mashariki

T L