• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
TUONGEE KIUME: Kutuma nauli na utapeli mwingine wa baadhi ya wanawake

TUONGEE KIUME: Kutuma nauli na utapeli mwingine wa baadhi ya wanawake

Na KELVIN KAGAMBO, Mwananchi Communications Limited

Kama hujawahi kutapeliwa na mwanamke, unastahili pongezi.

Takwimu tunazokusanya vijiweni tunakokutana wanaume zinasema wanawake wanaongoza kwa kututapeli.

Kama huna tafsiri iliyoshiba ya utapeli, basi ni hii; mtu anayejitwalia kitu kwa njia za udanganyifu.

Kwa mfano, ukimtaka mwanamke, ukampigia simu kumuomba aje nyumbani kwako, tena ukamuelezea waziwazi juu ya kila kinachoweza kutokea atakapofika kwako.

Akikubali lakini kwa sharti moja tu la kwamba umtumie nauli, na wewe ukatuma halafu asije, hapo umetapeliwa.

Ndiyo, kwa sababu amechukua pesa yako bila kufanya mlichokubaliana afanye.

Kama hujaelewa fikiria hivi; umeenda town kununua simu, ukakutana na muuza simu kwenye mojawapo ya maduka, akakwambia simu anayotaka kukuuzia ina intaneti, kamera na inakaa chaji wiki nzima, halafu akakuambia ili kuipata inabidi ulipe Sh10,000, ukangia mfukoni, ukalipa, ukapewa simu ukaondoka.

Kufika mbele unafungua unakuta kipande cha sabuni. Hata kama sabuni hiyo itakuwa na thamani ya Sh10,000 bado utakuwa umetapeliwa kwa sababu tu, mlikubaliana kuwa unanunua simu, sio sabuni kama ambapo ulituma nauli kwa makubaliano anakuja nyumbani na si vinginevyo.

Pia fikiria hivi; kwa sababu uko kwenye uhusiano naye, mwanamke anakwambia ‘baby maisha siku hizi ni kusaidiana, na mimi natafuta huku na wewe kule, mwisho wa siku tukiunganisha tunakuwa na kikubwa.

‘Kwa hiyo, naomba kama upambane tupate mtaji, nifungue biashara niwe na jambo la kufanya.’ Mwenyewe unakubali wazo, moyoni unasema mwanamke mwenye akili kama huyu nitampata wapi enzi hizi za wanawake wa mawigi na ‘make up’. Mwanamume unapambana, unaingia kulia, unatokea kushoto unakuja na mtaji na unampa aanze biashara.

Anaanza biashara na Mungu si Athumani, biashara inakubali, mambo yanaanza kuwa mazuri, mzee unakaa unasema sasa ule muda wa kuleta hamsini zangu na hamsini zake ili tupate mia umewadia, lakini badala yake huoni kitu, isipokuwa anakuja na mauzauza anaona kama hamuwezani, mnatakiwa tu mgawane ustaarabu, kila mtu achukue hamsini zake na mwenyewe anaondoka na kila kitu; hapa pia mzee baba umetapeliwa.

Umetapeliwa kwa sababu kama makubaliano yalikuwa ni muanzishe biashara ili faida iwe kwa ajili yenu wote, inakuwaje mtu anaondoka bila kutimiza makubaliano?

Na kuna huu utapeli wa kulipia ada, ni mbaya kuliko utapeli wowote ule. Unakuta mzee unajipinda kulipa ada za chuo, kununua vitabu na hela za intaneti, usisahau pocket money kama vile unasomesha binti yako, mwisho wa siku baada ya kuhitimu anakuchenjia, anakwambia naona mimi na wewe hatuendani, bora kila mtu afanye yake.

Sikia, hatusemi usiwe na mipango na mtu wako, hapana, isipokuwa ukae ukijua hawa watu na matapeli pia wamo.

  • Tags

You can share this post!

Umaarufu wa Raila na Azimio eneo la Maa wafifia, wa Ruto...

Zizi la Man United laungua nyota mwingine akipatwa na...

T L