• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Uhuru asisimua umati huku akimwalika Raila kuhutubu baada Naibu Rais

Uhuru asisimua umati huku akimwalika Raila kuhutubu baada Naibu Rais

RICHARD MUNGUTI na LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta, Jumanne alikiuka itifaki na kumwalika kinara wa ODM Raila Odinga baada ya Naibu Rais William Ruto kutoa hotuba yake wakati wa sherehe za Madaraka zilizofanyika jijini Kisumu.

Kwa kawaida, Bw Odinga alifaa kuzungumza kabla ya Naibu Rais Ruto ambaye katika miaka ya hivi karibuni ameonekana mgeni serikalini. Dkt Ruto alikamilisha hotuba yake iliyokuwa fupi kisha akamwalika Rais Kenyatta kutoa hotuba yake rasmi.

Wakati Rais Kenyatta alisimama kuhutubu, alimwita Bw Odinga ‘kusema machache’ huku akiomba radhi kwa kukiuka utaratibu wa itifaki.

“Mtaniwia radhi kwa kuvunja utaratibu leo ili nimwalike ndugu yangu, Raila Odinga, Jakom, awasalimie kisha atoe hotuba yake kuhusu Sikukuu ya Madaraka. Karibu ndugu yangu,” alisema Rais Kenyatta huku umati ukishangilia.

Alipoanza kuzungumza, Bw Odinga alimsifu Rais Kenyatta kwa kazi anayoendelea kufanya katika eneo la Nyanza. Bw Odinga pia alisifia matunda yaliyoletwa na handisheki. Kulingana na ratiba, jina la Bw Odinga halikuwa miongoni mwa wageni ambao wangehutubu.

Ratiba ilionyesha kuwa Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o alifaa kuzungumza na kisha kukabidhi usukani kwa Dkt Ruto ambaye baadaye angemwalika Rais.

Jumatatu, Bw Odinga ndiye alipokea Rais Ndayishimiye katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kisumu (KIA) saa 4:15 asubuhi.

Kulingana na utaratibu, Rais Ndayishimiye aliyeandamana na mkewe Angeline Ndayubaha, alifaa kupokelewa na Dkt Ruto au Waziri wa Mashauri ya Kigeni Raychelle Omamo.

Naibu wa Rais ambaye ametengwa serikalini, hajakuwa akishirikishwa katika mapokezi ya wageni wa serikali. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipozuru Kenya mwezi ja alilakiwa na mawaziri Bi Omamo na waziri wa Michezo Amina Mohamed.

You can share this post!

Walioteka mtoto walimpigia mama yake zaidi ya simu 70

Rais ashauri mahakama itumie hekima