• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Rais ashauri mahakama itumie hekima

Rais ashauri mahakama itumie hekima

JUMA NAMLOLA na RICHARD MUNGUTI

RAIS Uhuru Kenyatta ameitaka idara ya mahakama itumie hekima kubwa na kuzingatia utulivu wa kisiasa nchini inapojiandaa kusikiliza rufaa kuhusu BBI.

Alisema ijapokuwa kila mtu anapaswa kufuata sheria na kuheshimu uamuzi wa mahakama, ukuu na nguvu ya sauti ya mwananchi inafaa kutiliwa maanani.

Akizungumza Jumanne katika uwanja wa kimataifa wa michezo wa Jomo Kenyatta mjini Kisumu, Rais Kenyatta aliikumbusha idara ya mahakama kuwa uhuru ilio nao wafaa kutumiwa kwa uwajibikaji.

“Mahakama ilipofuta matokeo ya Uchaguzi wa Urais mwaka 2017, uchumi uliathiriwa. Tulipoteza shilingi trilioni moja kwa siku 123 pekee. Tulikuwa tunapoteza bilioni moja kwa kila saa. Wananchi watakuwa wakipoteza asilimia 30 ya bajeti ya taifa kila baada ya miaka mitano kwa sababu ya siasa chafu,” akasema.

Wakati wa sherehe hizo za Madaraka zilizohudhuriwa na Jaji Mkuu Martha Koome, Rais Kenyatta aliitaka Mahakama ijiulize maswali kuhusu njia za kurekebisha siasa mbaya. “BBI inalenga kuwaleta watu pamoja, kuunda siasa zinazojumuisha pande zote, na kumaliza uongozi wa makabila mawili. Ikiwa Mahakama inajali haya, basi yapaswa ijiulize kama uamuzi wa Mahakama Kuu kutupa mswada wa marekebisho ya Katika (2020) almaarufu BBI unazingatia haya,” akasema.

Alikumbusha kwamba Wakenya wamekuwa wavumilivu kuhusiana na maamuzi ya mahakama, lakini safari hii suala lililo mbele ya mahakama ya rufaa lina athari kubwa kisiasa na kiuchumi.

Rais Kenyatta na kinara wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga tayari wameandaa rufaa zao kupinga uamuzi uliotolewa Mei 13 na majaji watano.

Majaji Teresia Matheka, George Odunga, Joel Ngugi, Chacha Mwita na Jairus Ngaah walisema kuwa kifungu cha 257 cha Katiba hakikufuatwa katika mchakato wa kuifanyia mageuzi Katiba.

Kifungu hicho kinasema kwamba marekebisho ya Katiba kupitia juhudi za Wengi, yafaa kuanzishwa na wananchi wenyewe, ambapo watu milioni moja watatia saini pendekezo. Kulingana na majaji hao, kwenye mswada wa BBI, ni Rais aliyeanzisha mchakato huo.

Mahakama ya rufaa inatarajiwa leo Jumatano kutoa mwelekeo wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Rais wa Mahakama ya Rufaa Jaji Daniel Musinga aliamuru kesi hiyo itajwe mbele ya majaji watatu.

Majaji hao wataelekeza jinsi rufaa hiyo itakavyosikilizwa.

Mawakili wa Rais Kenyatta na Bw Odinga, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na mwanasheria mkuu, waliagizwa wafike kortini saa tatu asubuhi.

Bw Odinga anawakilishwa na wakili Paul Mwangi.

Wengine watakaofika mahakamani ni walalamishi waliowasilisha kesi hiyo katika mahakama kuu, miongoni mwao ni mtaalamu wa masuala ya uchumi David Ndii.

Kupitia msajili wa idara ya mahakama ya rufaa Bw Moses Serem, Jaji Musinga siku ya Ijumaa aliamuru wahusika wote wafike kortini Jumatano kupata maagizo.

“Rufaa zilizowasilishwa sitasikilizwa Juni 2, 2021 kutoa mwelekeo iwapo maombi yaliyowasilishwa yatasikizwa kwanza ama rufaa kamili itaanza kusikizwa moja kwa moja,” alisema Bw Serem katika arifa aliyopelekea mawakili wanaohusika.

Jaji Musinga alisema mahakama itatoa mwelekeo iwapo rufaa kamili itasikizwa ama ni maombi ya kuzima kusikizwa kwa kesi hiyo.

You can share this post!

Uhuru asisimua umati huku akimwalika Raila kuhutubu baada...

Huzuni pacha wakifa baharini