• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:50 AM
Ujenzi kando ya Mto Ngong waelekeza maji katika shule ya Songa Mbele

Ujenzi kando ya Mto Ngong waelekeza maji katika shule ya Songa Mbele

Na SAMMY KIMATU

ONGEZEKO la ujenzi wa nyumba za orofa katika mtaa mmoja wa mabanda kunatishia usalama wa Shule ya watoto wanaoishi na ulemavu iliyoko katika kaunti ndogo ya Starehe.

Hayo yalisemwa Jumatano na Usimamizi wa Mukuru Promotion Centre (MPC) – kituo kinachofadhili familia maskini katika maeneo ya Mukuru.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa MPC, Mtawa Mary Killeen, taasisi ya Songa Mbele na Masomo katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kisii, South B iko katika njia panda.

Hii ni baada ya tetesi kwamba wanyakuzi wa ardhi wamejenga nyumba za orofa ndani ya mto Ngong na kulazimisha maji kuelekea shuleni.

“Watu binafsi wamejenga nyumba za mawe zenye orofa ndani ya mto Ngong katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba na kulazimisha maji kuchukua mkondo mwingine. Kwa sasa, maji mtoni yamesukumwa hadi kwenye ukuta wa shule yetu ya walemavu,” mtawa Mary akaambia Taifa Leo.

Kinachokera MPC zaidi ni kwamba shule ya Songa Mbele imewasajili watoto kutoka mitaa mbalimbali ya mabanda katika maeneo hayo.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi ndio wanaochangia katika masuala ya kutatiza shughuli za kiofisi katika kituo cha MPC.

Kwa mujibu wa mdokezi wa Taifa Leo, yamkini ujenzi wa nyumba kwenye mitaa hiyo umekumbwa na sakata iliyo na historia ndefu.

“Mabwanyenye huuziwa ploti na wazee wa mitaa wanaoshirikiana na maafisa wa utawala. Mwanzoni, walikuwa wakijenga nyumba za mabati (muda) wakihofia zitabomolewa na serikali wakati wowote,” mdokezi wetu asema.

Fauka ya hayo, ni kutokana na nafasi za ardhi kuadimika siku hizi ambapo wamebadili mbinu.

“Wakati huu, mabwanyenye hununua nyumba zilizojengwa zamani kwa mabati kisha huzibomoa na kujengwa za kisasa zilizojengwa kwa mawe na za orofa,” mfichuzi akasema.

Maafisa wa utawala waliopo ofisini siku hizi wakiwemo manaibu wa machifu, machifu sawia na mkuu wa tarafa ya South B, Bw Michael Aswani Were walijitenga kando na suala hili.

Wakijitetea, walisema hawana thibitisho kwamba utawala wa awali ulihusika katika sakata hiyo wakiongeza kuwa wao ni wageni na walikuta mitaa ikiwa na nyumba za orofa.

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Sahihi ni ‘Hamjambo’ wala si...

Mathare North All Stars na Kapsambo waibuka mabingwa NCFA

T L