• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
Mathare North All Stars na Kapsambo waibuka mabingwa NCFA

Mathare North All Stars na Kapsambo waibuka mabingwa NCFA

Na PATRICK KILAVUKA

Mathare North All Stars na Kapsambo walinyanyua taji la Ligi ya Primia na Daraja ya Kwanza ya Shirikisho la Soka Kaunti ya Nairobi (NCFA) mtawalia.

Mathare walitawazwa baada ya kucheza mechi yao ya mwisho Jumapili, uwanjani BP na kuandikisha sare ya 1-1 dhidi ya Amazon Tigers na kuvuna alama 55. Katika usanjari huu, walifuatwa na Angaza A (40) na ya tatu bora Kwangware All Stars (39).

Timu zingine ambazo zilishiriki katika kinganganyiro cha ligi hiyo ni GSU United (38), Komarock Youth (38), South City (37), Amazon Tigers (35), Zion Winners (30), Egesa (26), Gava (25), Utalii na Garden Ego (23) kila moja na mkiani walikuwa Kassmatt (22).

Kapsambo waliibuka mabingwa wa Ligi ya Daraja ya Kwanza kwa kuzoa alama 20, wakafuatwa na Kinyago United (16) na wa tatu bora walikuwa Westlands Soccer (11). Wengine walikuwa Locomotive na Bufallo (7) kila moja, Sodom (4) na waliofunga jedwali walikuwa Golden Stars (1).

Mathare North All Stars walipokea Sh100,000, sare, mpira na cheti hali kadhalika Kapsambo ambao waliotia fora waliweka kibindoni Sh50,000, jezi, mpira na cheti. Timu zote ambazo zilishiriki zilipokea jezi, mpira na cheti cha ushiriki.Kinara wa ligi hiyo Charles Njoroge, alisema licha ya changamoto kuwepo ligi ilimalizika tangu kuanzishwa machi, 2021.

“Tumekuwa na changamoto kuu ya fadhili, idadi ya idadi ndogo ya timu kujisajili kwa kutokuwa na wadhamini, viwanja vya kuchezea mechi za ligi kwani vingi vilikuwa vinatumiwa na Ligi za FKF na enzi isiokuwa ya kawaida ya corona kutatiza uendelezi wake. Lakini tunashukuru Mungu kutuwezesha ilikamilika,” afichua mwenyekiti huyo.

Alishukuru wadau wa jopokazi ambao walishirikiana sako kwa bako katika kufanikisha ligi hiyo. Aliongezea kwamba anapongeza pia timu ambazo zilijitolea kucheza ngarambe hiyo na kuhudhuria mechi pasi na kuchelea hadi zikatamatika.

Alidokeza kwamba walionesha uanaspoti katika kudumisha uhai wa soka hususa wakati huu mgumu ambapo changamoto zilikuwa nyingi. “Ninatazamia wafadhili watajitokeza kuunga mkono kazi hii ya kukuza Vipaji vya soka mashinani kwa sababu kizingiti katika ukuzi wa spoti nchini ni udhamini na kujitolea,” akadokeza.

Pia, aliaarifu kwamba anatazamia timu kuongezeka msimu ujao kwani ni ligi ambayo imeandikishwa Kauntini rasmi.

You can share this post!

Ujenzi kando ya Mto Ngong waelekeza maji katika shule ya...

Mshukiwa wa ujambazi auawa kwa kupigwa risasi na polisi...

T L