• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
NDIVYO SIVYO: Sahihi ni ‘Hamjambo’ wala si ‘Hamjamboni’

NDIVYO SIVYO: Sahihi ni ‘Hamjambo’ wala si ‘Hamjamboni’

Na ENOCK NYARIKI

DHANA nyingine inayokaribiana na ile ya viwakilishi nafsi tuliyoijadili awali inahusu kiambishi {hu}.

Hiki huwa na dhima mbili ambazo zitatusaidia kuelewa kwa nini ni kosa kusema *hamjamboni.

‘Hu’ hutumiwa kuonyesha hali ya mazoea. Mfano: Hamisi huenda shuleni kila siku. Viambishi vinavyowakilisha hali havibainishi wakati mahususi wa kutendeka kwa kitendo. Huonyesha tu kuwa kitendo kimo katika hali fulani ya wakati uliopo, uliopita au ujao.

Aghalabu, maelezo zaidi huhitajiwa ili kuonesha nyakati zinazozungumziwa.

{Hu} pia hutumiwa kukanusha nafsi ya pili umoja. Mifano: Wewe ulisoma (uyakinishaji); Wewe hukusoma (ukanushaji). Katika mifano hii, kiambishi {u} cha uyakinishaji hubadilika na kuwa {hu} cha ukanushaji. Hiyo ni njia rahisi ya kuelezea badiliko hilo bila kujikita katika mifanyiko ya sauti.

‘Hamjambo’ ni wingi wa ‘hujambo’. Salamu hizi hutumiwa wakati wowote wa siku.

Yamkini neno ‘hujambo’ ni ufupisho wa maneno: ‘huna’ na ‘jambo’. Anayemwamkia mwenzake ‘huna jambo?’ yaani ‘hujambo?’ hutaka kupata uthibitisho kwamba kweli anayesalimiwa yu mzima.

Kwa hivyo, kauli ‘sijambo’ ambayo yamkini pia imetokana na ‘sina jambo’ ni itikio (response) la salamu hizo.

Kufikia hapa, tumeeleza kuwa ni kosa kusema *hamjamboni ila hatujatoa sababu.

Kiambishi {m} katika maamkizi ‘hamjambo’, kinawakilisha mtendwa ambaye katika muktadha huu yuko katika nafsi ya pili wingi. Viambishi {ha}’ na {m} ni wingi wa {hu}.

Kwa hivyo, kusema ‘hamjamboni’ ni kosa la kutumia kiambishi {ni} cha wingi na viwakilishi nafsi vinavyotekeleza dhima hiyo hiyo ya wingi.

You can share this post!

KAULI YA MATUNDURA: Jinsi ya kumtambua mwandishi chipukizi...

Ujenzi kando ya Mto Ngong waelekeza maji katika shule ya...

T L