• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Unyakuzi watishia faida za misitu ya Kaya

Unyakuzi watishia faida za misitu ya Kaya

Na SIAGO CECE

UNYAKUZI wa misitu ya Kaya Pwani umetishia kuvuruga mpango wa serikali kuitumia kama vituo vya utalii.

Wazee wa Kaya wamekumbwa na wasiwasi wakisema tayari kuna mabwanyenye ambao wameanza kuingilia misitu hiyo yenye thamani kubwa kwa jamii ya Wamijikenda.

Kuna zaidi ya misitu 30 inayohifadhiwa na serikali kama turathi za kitaifa.

Akiongea katika Msitu wa Kaya Kinondo, mzee wa Kaya hiyo, Bw Suleiman Gombo alitaka unyakuzi na uharibifu wao ukomeshwe kwa manufaa ya jamii.

“Watu wengi tayari wanaingia katika misitu hii na kuinyakua kinyume na sheria. Hii inaweka misitu yetu katika hatari ya kupoteza thamani yake,” Bw Gombo alisema.

Wizara ya Utalii tayari imeanza mipango ya kujumuisha Kaya kama vivutio vya utalii, mbali na fuo za bahari na mbuga za wanyama maeneo ya Pwani.

Mbali na unyakuzi, Kaya nyingi pia ziko hatarini kwa kuwa idadi ya watu wanaokata miti ya kuchoma makaa inaongezeka.

Kulingana na msimamizi wa Idara ya Turathi za Kitaifa (NMK), tawi la Kwale, Bw Matano Abdulrahman, misitu ya Kaya itafanyiwa usoroveya upya ili kupunguza athari za kunyakuliwa.

“Kuna visa vingi vya unyakuzi wa ardhi hivi sasa katika Kaunti ya Kwale na ni lazima mipaka ya Kaya ipimwe tena. Bila hiyo watu binafsi watadai kuwa ni mashamba yao,” Bw Abdulrahman alisema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii, Bi Safina Kwekwe, alisema maeneo ya Kaya yanaweza kutumiwa kuvutia watalii na hivyo kuchangia katika kuinua uchumi wa Pwani na taifa kwa jumla.

“Tutashirikiana na wizara na wadau wengine kuhakikisha kuwa eneo la Pwani limepata mapato kutokana utalii wa misitu ya Kaya,” Bi Kwekwe alisema akiongea katika Kaya Kinondo

You can share this post!

Raila atetea mali fiche ya Uhuru

AKILIMALI: Maparachichi aina ya hass yamvunia kipato katika...