• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 PM
AKILIMALI: Maparachichi aina ya hass yamvunia kipato katika kipande kidogo cha ardhi mjini Ogembo

AKILIMALI: Maparachichi aina ya hass yamvunia kipato katika kipande kidogo cha ardhi mjini Ogembo

Na RICHARD MAOSI

KILIMO cha parachichi kimewafaa wengi wanaojishirikisha nacho kama kilimo-biashara, mbali na manufaa mengi kwa mwili wa binadamu.

Kuna aina nyingi ya parachichi, mojawapo ikiwa ni ile inayotambuliwa kama hass na ambayo imeibuka kuwa maarufu miongoni mwa wanaofanya kilimo-biashara.

Akilimali ilipata fursa ya kuzuru eneo la Ogembo katika barabara ya Kilgoris ukielekea Kisii ambapo tulikutana na mkulima Fred Omoke, aliyewekeza kilimo cha parachichi aina ya hass.

Kulingana naye, wakulima wengi walikuwa wakitegemea kahawa na majanichai, ila bei ya bidhaa hizi iliporomoka kimataifa na kuwalazimu kusaka njia mbadala ya kujiendeleza kimaisha.

Anasema awali alikuwa akikuza miparachichi ya kiasili kuzaa matunda kwa matumizi ya nyumbani tu, ambayo kwa kawaida huwa mirefu na huchukua muda mrefu kukomaa kiasi kwamba mkulima hawezi kupata tija kwa wakati.

Kuanzia alipostaafu aliamua kuelekeza nguvu zake zote kwenye kilimo ambapo anakuza ndizi, mipapai ni mboga ya mchicha katika kipande cha ardhi ya robo tatu hivi.

Kutokana na azma yake kufanikiwa alijibidiisha kuzuru maonyesho ya kilimo ikiwa ni pamoja na kutangamana na wataalam, ambapo alipata ujuzi ndiposa akaamua kuanzisha mradi wa parachichi aina ya hass.

“Katika kipindi cha miaka mitano hivi kila mti unaweza ukakupatia idadi ya wastani ya parachichi zisizopungua 1000,” anasema.

Akiwa mmoja wa wakulima wengi wanaochuma riziki kutoka kwa aina hii ya parachichi, anaungama kuwa bei ya sokoni mara nyingi huwa ni kati ya Sh10-32 kulingana na kiwango cha ubora wa tunda.

Hii ikimaanisha kuwa mkulima anaweza kutengeneza zaidi ya Sh100,000 kila msimu kwa kumiliki miti mitatu tu ya kuzaa parachichi aina ya hass.

Aidha anasema kuwa matunzo yake huwa ni rahisi ikizingatiwa kuwa miti yake huwa ni mifupi hivyo basi ni mazao ambayo yanaweza kukua baina ya mimea mingine.

Pia humsaidia mkulima kukabiliana na ndege ambao wanaweza kumsababishia hasara mara tu mazao yake yanapokuwa tayari kabla ya kuvuna.

Anasema kuwa mbolea ya kupandia inayohitajika inaweza kuwa ile ya kiasili kama vile samadi na mchanganyiko wa aina nyingine ya mboji au ya viwandani lakini kwake mara nyingi anatumia samadi.

Ambapo kiasi cha kilo 16-20 huwekwa katika kila shimo miezi mitatu kabla ya kupanda miche.

Kinyume na miparachichi ya kiasili ambayo huchukua hadi miaka minane kabla ya kukomaa, miparachichi ya kisasa aina ya hass huchukua miaka mitatu kuanza kuzaa maparachichi na miezi mingine sita kabla ya kukomaa.

Alieleza kuwa parachichi huchukua hadi miezi saba mtini kukomaa. Omoke anasema kuwa kwa mara ya kwanza mti wa hass unaweza kubeba matunda baina ya 70-120 lakini idadi yake huendelea kuongezeka kadri miaka inavyosonga.

“Mti wa parachichi unapofikisha miaka mitano hivi huwa umekomaa kabisa na mkulima anaweza kupata matunda kuanzia 1, 200 hivi kila msimu.”Anaongeza kuwa kuwa wanunuzi wake wengi ni wauzaji katika soko la Ogembo, Kilgoris, Nakuru na Kisii.

You can share this post!

Unyakuzi watishia faida za misitu ya Kaya

AKILIMALI: Pilipili kali inayoogopwa na wenyeji kwa mwasho...