• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Urithi wa Mvurya waibua joto zaidi

Urithi wa Mvurya waibua joto zaidi

Na MOHAMED AHMED

SIASA za kurithi kiti cha ugavana Kaunti ya Kwale zimeanza kupamba moto huku naibu Gavana wa Kwale Fatuma Achani na mbunge wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani ambao wote wanakimezea mate kiti hicho wakirushiana cheche za maneno ya kisiasa.

Haya yanajiri mwezi mmoja tu baada ya viongozi hao wawili kuungana na kumfanyia kampeni kabambe mbunge wa sasa wa Msambweni Feisal Bader ambaye alishinda kiti hicho mwezi Disemba.

Licha ya kuungana kwao wakati huo, sasa kila mmoja anavutia kwake na kuanza kutiana kucha kwa kutaka kumrithi Gavana Salim Mvurya ambaye pia ameonekana kulemea upande wa Bi Achani.

Bi Achani ndiye naibu gavana pekee katika kanda ya Pwani ambaye amehudumu mihula miwili chini ya mkuu wake Bw Mvurya.

Katika ziara ya Naibu Rais William Ruto iliyomalizika Jumapili hii, Bw Mwashetani alikuwa akimfokea Bi Achani.

Mara ya kwanza, alimlaumu kwa madai ya kujaribu kutatiza mkutano wa kwanza wa Dkt Ruto eneo la Mwangulu ambapo mbunge huyo ndiye aliandaa.

Alidai kuwa siku hiyo, Bi Achani alijaribu kuambia wakazi wasiende kwenye mkutano huo. Hata hivyo Bi Achani amepinga madai hayo.

“Kuna viongozi wengine wanasubiri kuidhinishwa lakini mimi sisubiri hilo. Tutapambana na yeye 2022. Dunia hii mpaka ujitume na sio kusubiri kuidhinishwa,” akasema Bw Mwashetani.

Akizungumza katika mkutano mwingine eneo la Kinango, Bw Mwashetani alidai kuna viongozi ambao wanatukana wenzao.

“Kwale ni yetu sote na sisi lazima tujitahidi tuhakikishe tunaleta mabadiliko ndani ya kaunti hii,” akasema.

Hata hivyo, akizungumza na wanahabari eneo la Show Ground, Bi Achani alisema kuwa anashangazwa na maneno ya Bw Mwashetani ambaye amemuweka mdomoni kana kwama ni yeye pekee ndiye anayetaka kiti cha ugavana.

Bi Achani ambaye alizungumza mbele ya Bw Mvurya alisema kuwa yeye hatasubiri kuidhinishwa na kiongozi yeyote bali utendakazi wake ndio utakaowapa fursa wakazi kuchagua.

“Kupata kura itategemea na mwananchi wa Kwale. Sisi tunafanya kazi na wananchi na sio kusubiri kuidhinishwa na kiongozi yoyote wa kitaifa,” akasema Bi Achani.

Kuhusiana na madai ya kutatiza mkutano wa Kwale, Bi Achani alisema yeye hakufika hapo na siku hiyo alikuwa eneo la Vigurungani ambao alikuwa anaongoza shughuli ya kutoa msaada wa fedha za kusaidia masomo.

You can share this post!

Afueni kwa Sonko akipata dhamana ya Sh300,000 lakini…

TAHARIRI: Elimu: Mtaala mpya wahitaji ushirikiano