• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Vijana wakosolewa kupenda bodaboda badala ya masomo

Vijana wakosolewa kupenda bodaboda badala ya masomo

STEPHEN ODUOR NA MAUREEN ONGALA

MBUNGE wa Galole, Bw Said Hiribai, amewakosoa vijana wa Tana River ambao huchagua biashara ya bodaboda badala ya kutumia nafasi walizotengewa katika vyuo vya kiufundi kujielimisha.

Mbunge huyo alisema serikali ya kitaifa ilitenga pesa za kufadhili masomo ya vijana katika vyuo hivyo na kuna ufadhili mwingine kutoka kwa maeneobunge ilhali vijana wamekataa kujisajili.

Kulingana naye, kazi nyingi hutokea katika kaunti na maafisa hulazimika kutafuta wataalamu kutoka nje kwa sababu walio na ujuzi wa kiufundi hawapatikani katika kaunti hiyo.

Chuo cha mafunzo ya kiufundi cha Hola kina wanafunzi wasiozidi 200 tangu kilipofunguliwa Februari 2021.

Hali sawa na hii imekuwa ikishuhudiwa katika kaunti nyingine mbalimbali za Pwani.

Waziri wa Elimu katika Kaunti ya Kilifi, Bi Rachael Musyoki, hata hivyo alisema hamasisho limeanzishwa kuongeza idadi ya vijana wanaojiunga na taasisi hizo.

“Vijana wetu hawataki kusomea mafunzo yanayochukua muda mrefu. Tulianzisha kozi za muda mfupi na vijana sasa wanajiandikisha, kumaanisha wameanza kufahamu kwamba taasisi hizi si za waliofeli masomoni ,” akasema.

Takwimu zimeonyesha kuwa idadi ya wanafunzi iliongezeka kutoka 3,000 hadi 5,400 katika miaka miwili iliyopita ilhali vijana takriban 10,000 wamekuwa wakilengwa Kilifi pekee.

Hivi majuzi, mkuu wa chuo cha ufundi cha Weru, Kaunti ya Kwale, Bw Edward Mwagambo alisema kati ya jumla ya wanafunzi 780 katika chuo hicho cha ufundi, 150 pekee ni wenyeji.

Chuo hicho kina uwezo wa kusajili wanafunzi 1,500.Hapo awali, aliyekuwa katibu wa vyuo vya ufundi nchini chini ya Wizara ya Elimu, Bw Kevit Desai alielezea masikitiko yake kutokana na idadi ndogo ya vijana wanajiounga na vyuo hivyo katika eneo la Pwani.

Katibu huyo alitoa mfano wa chuo kimoja katika Kaunti ya Kwale kilicho na uwezo wa kuwa na wanafunzi 1,000 lakini kilikuwa na wanafunzi 13 pekee.

  • Tags

You can share this post!

Familia yapinga mshukiwa wa mauaji ya baba yake kupewa...

Mwanahabari wa michezo kuzikwa kesho Kakamega

T L