• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Viongozi Mlimani lawamani kwa ‘kuwa waoga’ kuwatetea raia

Viongozi Mlimani lawamani kwa ‘kuwa waoga’ kuwatetea raia

NA WANDERI KAMAU

ALIYEKUWA Gavana wa Nakuru, Bw Lee Kinyanjui, ameonya kwamba huenda eneo la Mlima Kenya likaachwa nyuma kimaendeleo, ikiwa viongozi waliopo hawatapigania utekelezaji wa mfumo utakaohakikisha kuwa pesa za umma zinagawanywa kulingana na idadi ya watu.

Bw Kinyanjui alisema hatua ya viongozi kuendelea kunyamazia utekelezaji wa mfumo huo, utalifanya eneo hilo kubaki nyuma kiuchumi, hasa katika sekta ya kilimo, licha ya kuwa na mgao mkubwa katika serikali ya Rais William Ruto.

“Haijalishi idadi ya nyadhifa tunazoshikilia serikalini. Mfumo wa Mtu Mmoja-Kura Moja-Shilingi Moja ndiyo njia pekee itakayohakikisha wenyeji wa Mlima Kenya wamefaidika kutokana na idadi yao kubwa. Sisi tunajumuisha angaa asilimia 35 ya watu kote nchini. Tunafaa kupata haki yetu,” akasema Bw Kinyanjui, jana asubuhi, kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio.

Kiongozi huyo, ambaye alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakimpigia debe kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, katika eneo hilo mwaka uliopita, alisema ni wakati viongozi waliopo wapiganie ufufuzi na utekelezaji wa mfumo huo, hasa baada ya Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI) kutupiliwa mbali na mahakama.

“Bila shaka, BBI ndiyo ilikuwa na ‘tiba’ kwa wenyeji wa ukanda huu, kwa kuhakikisha kiwango cha pesa ambazo wamekuwa wakigawiwa na Serikali ya Kitaifa kimeongezeka. Nilipokuwa gavana, nilienda katika baadhi ya kaunti, na kubaini kuwa mwanafunzi mmoja anaweza kupata hadi Sh100,000 kama basari. Hata hivyo, hali ni kinyume katika eneo hili, kwani wazazi hung’ang’ana kuhakikisha wanafunzi wao wamepata angaa basari ya kati ya Sh2,000 na Sh5,000. Huu ni mtindo unaofaa kubadilishwa. Ni ubaguzi wa wazi,” akasema Bw Kinyanjui.

Kauli ya kiongozi huyo inajiri siku chache baada ya mbunge Gathoni Wamucomba wa Githunguri, kudai kwamba waliagizwa na uongozi wa Kenya Kwanza kunyamazia mfumo huo, kwenye kikao kimoja kilichofanyika katika Ikulu ya Nairobi.

Jumapili iiyopita, Bi Wamucomba alidai kuwa agizo hilo ndilo limewafanya viongozi wengi wa Mlima Kenya kunyamazia mfumo huo, licha ya kuwa miongoni mwa masuala makuu walioahidiwa na Rais William Ruto.

Bi Wamucomba alisema kuwa “uoga ambao unaonekana kuwaingia wabunge kutoka ukanda huo, ndio umemfanya kujitokeza kushinikiza utekelezaji wa mfumo huo.”

“Ikiwa tutaendelea kunyamaza, ni nani atawatetea watu wetu? Ni lini kutakuwa na usawa ikiwa mfumo huu hautatekelezwa wakati huu tunaodai kuwa na mgao na usemi mkubwa serikalini? Hata kama nitakuwa peke yangu, nitafanya kila niwezalo kuhakikisha mfumo huu umeanza kutekelezwa,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Mkuu wa polisi Makadara athibitisha maafisa wa DCI...

Washukiwa wa wizi wa vipande vilivyokatwa kutoka kwa magari...

T L