• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Washukiwa wa wizi wa vipande vilivyokatwa kutoka kwa magari na vifaa vya kielektroniki waachiliwa kwa dhamana

Washukiwa wa wizi wa vipande vilivyokatwa kutoka kwa magari na vifaa vya kielektroniki waachiliwa kwa dhamana

NA TITUS OMINDE

WASHUKIWA sita wa kuiba na kubomoa magari na kuuza vipande katika mji wa Eldoret na viunga vyake, wameachiliwa Ijumaa kila mmoja kwa dhamana ya Sh10,000 pesa taslimu huku uchunguzi ukiendelea.

Washukiwa hao ambao ni pamoja na kiongozi wa wanawake kutoka kanisa la Akorino, walikamatwa katika mtaa wa Kapsoya viungani mwa mji wa Eldoret kufuatia taarifa kutoka kwa umma.

Wakiwa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Rosemary Onkoba, washukiwa hao hawakusomewa mashtaka kwani polisi waliieleza mahakama kuwa bado hawajakamilisha uchunguzi.

Uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa magari yaliyobomolewa yalikuwa yameibwa kutoka kaunti jirani.

Huku akiwasilisha ombi la kuwazuilia washukiwa hao, afisa wa uchunguzi Rosemary Nyokabi kutoka kituo cha polisi cha Naiberi aliambia mahakama kuwa wapelelezi bado hawajakamilisha uchunguzi hivyo basi walihitaji muda zaidi kukamilisha uchunguzi kabla ya kuwafungulia mashtaka washukiwa ipasavyo.

Kupitia hati yake ya kiapo, Bi Nyokabi aliambia mahakama kuwa ingawa mashahidi wakuu hawakuwa wameandika taarifa, wamiliki wa mali iliyoibwa bado hawajatambuliwa.

Bi Nyokabi aliambia mahakama kuwa polisi bado hawajabaini umiliki wa magari hayo kupitia Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Uchukuzi (NTSA).

Mahakama pia iliambiwa kuwa washukiwa hao pia walikutwa na bidhaa za kielektroniki zinazoshukiwa kuibiwa ambazo ni pamoja na, televisheni, redio, wenyewe bado hawajatambua bidhaa hizo.

Mawakili wanaowawakilisha washtakiwa walipinga kuwekwa kizuizini kwa madai kuwa ni mbinu ya kuendelea kutesa wateja wao bila sababu.

“Wateja wangu walikuwa wamezuiliwa katika kituo cha polisi cha Kapsoya kwa muda zaidi ya inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria. Maafisa wangetumia kipindi walichokuwa rumande kukamilisha uchunguzi,” alisema wakili Ignatius Mwaka huku akipinga ombi hilo.

Hakimu aliamuru washukiwa hao waachiliwe kwa dhamana ya pesa taslimu Sh10,000 kila mmoja wakisubiri uchunguzi.

Akitoa uamuzi huo, hakimu alisema upande wa mashtaka ulikosa sababu za msingi za kuwaweka watuhumiwa hao kwa muda uliotajwa wa siku 10.

“Ombi la upande wa mashtaka haliridhishi kuazulia washukiwa kwa siku kumi, kwa hiyo nawaachilia washukiwa kwa dhamana ya pesa taslimu sh10,000,” aliagiza hakimu.

Aidha hakimu aliamuru washukiwa wawe wakiripoti katika kituo cha polisi mara moja kwa wiki au wakati wowote wanapotakiwa na polisi.

Kesi hiyo itatajwa Oktoba 23, 2023.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi Mlimani lawamani kwa ‘kuwa waoga’...

Sakaja afufua shughuli za kaunti kwa kutia saini mswada wa...

T L