• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Vituo vya pombe vyaongeza uzembe Juja

Vituo vya pombe vyaongeza uzembe Juja

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Witeithie, Juja, Kaunti ya Kiambu, wanalalamika kuhusu ongezeko la vituo vya kuuza pombe kali ya whisky.

Katika mkutano ya washika dau wa sekta tofauti na wamiliki wa baa eneo hilo, wakazi hao walisema hali hiyo imesababisha vijana wengi kupotelea ulevini bila kufanya kazi.

Afisa msimamizi wa kaunti ndogo ya Juja, Bi Selline Muriithi, alisema kuna haja ya kila mmoja kuendesha biashara halali bila kutafuta mikato.

Afisa wa usimamizi wa kaunti ndogo ya Juja, Bi Selline Muriithi akihutubia washika dau eneo la Witeithie, Kaunti ya Kiambu. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Uchunguzi uliofanywa majuzi umebainisha maskani hizo za pombe zinawauzia hata vijana wa shule pombe ya mvinyo aina ya whisky, jambo alilosema linachora taswira mbaya.

Alisema maafisa wa usalama wataanza kupiga doria katika kumbi za uuzaji pombe ili kuwasaka hasa vijana wa shule ambao huonekana maeneo hayo.

“Tutafanya juhudi kuona ya kwamba wanaokata leseni pekee ndio watakaoruhusiwa kufanya biashara hiyo ya pombe,” alifafanua afisa huyo.

Alieleza uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa kuna sehemu 50 zinazoendesha biashara ya pombe na nyingi hazina leseni maalum.

Ilidaiwa pia kuwa maskani hizo zimegeuzwa maficho ya wahuni.

Alisema wamejadiliana na vitengo vya usalama kuwa kutakuwa na ulinzi wa maeneo hayo kwa muda wa saa 24 kutokana na vitisho vya ugaidi ambayo inaendelea kutisha nchi yetu.

Wamiliki wa baa wameshauriwa kuzingatia sheria na kanuni za kuzuia Covid-19, ili kuzuia usambazaji wa corona hata wakati huu ambapo kafyu iliondolewa na serikali.

Chifu wa eneo la Witeithie, Juja, Bw Muchui Muiruri alisema hivi majuzi mwanafunzi alinaswa katika maskani ya pombe akibugia pombe yenyewe.

Alisema watafanya msako kuvamia maskani nane za kuuzia pombe ambazo zinashukiwa hazijakata leseni.

“Hatutaki kuchukulia mambo kwa wepesi lakini ni sharti tuwanase wale wanaokiuka sheria,” alisema chifu huyo.

  • Tags

You can share this post!

Mna siku 7 kumshtaki Mwendwa, korti yaagiza

Wasichana chipukizi wa ACUWM watamba mbio za nyika

T L