• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Wasichana chipukizi wa ACUWM watamba mbio za nyika

Wasichana chipukizi wa ACUWM watamba mbio za nyika

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

JOSEPHINE Sampaiyo aliwaongoza wasichana wenzake watatu wa kambi ya riadha ya Athletics Camp Under White Moutain (ACUWM) kushinda Mbio za Nyika zilizofanyika viwanja vya shule ya upili ya Kimana Girls Secondary juzi Jumatano.

Josephine, mwanafunzi wa darasa la sita wa shule ya msingi ya Winners Academy ya mjini Kimana alikamkilisha mbio za kilomita tano kwa muda wa dakika 17 nukta 11 akifuatiwa na mwanafunzi wa darasa lake wa shule hiyo, Maria Shali aliyetumia dakika 18:20.

Na wanariadha wengine wawili wa kambi hiyo inayomilikiwa na raia wa Marekani Derick Stuj, wanafunzi wa shule ya upili ya Kimana Girls, Philes Malemba na Agnes Mwashigadi walifanikiwa kumaliza nafasi za tatu na nne kwa kutumia dakika 18:56 na 18:59 mtawalia.

Maria, Philes na Agnes waliotoka Kaunti ya Taita Taveta walijiunga na kambi hiyo ya riadha mwaka huu na kuanza kupata mazoezi ya mbio ndefu kutoka kwa kocha Boniface Nduva ambaye mwenyewe ni mwanariadha anayeshiriki mbio za marathon za kimataifa.

Mkurugenzi wa kambi hiyo, Robert Saruni amesema anafurahikia jinsi wasichana hao wanavyoendelea kufanya vizuri katika mbio na akawa na matumaini wanaweza kuwa wakimbiaji mahiri miaka ijayo. Alisema msichana mwingine wa tano ambaye yuko katika kambi hiyo kutoka Taita Taveta, Jardeen Malemba hakuweza kushiriki kwenye mbio hizo sababu alikuwa mgonjwa.

Kwenye mbio za mita 1,500, Josephine alionyesha umahiri wake kwa kuibuka mshindi alipotumia dakika 4:45 akifuatiwa na Maria aliyemaliza kwa dakika 4:56 hali Agnes Mwashighadi akitosheka na nafasi ya tatu kwa kutumia 5:05. Kocha wa kambi hiyo ya ACUWM, Boniface Nduva amewapongeza wanariadha wake kwa kufanya vizuri kwenye mbio hizo na akaeleza matumaini yake kuwa kila watakapokuwa wakubwa, watazidi kuimarika.

“Ninataka washiriki kwenye mbio zitakazofanyika ili waweze kupata uzoefu. Nia kubwa ya kambi yetu ni kuhakikisha wanariadha wetu wanatamba kuanzia mashinani hadi kwenye mashindano ya kitaifa na kimataifa,” akasena Nduva.

Mwisho

You can share this post!

Vituo vya pombe vyaongeza uzembe Juja

kinoti kufungwa miezi minne gerezani

T L