• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:55 AM
Vyuo vinavyotoa mafunzo ya kilimo vyahimizwa kuwa na kozi fupi za masomo kunoa zaidi wanafunzi, mbali na taaluma wanazosomea

Vyuo vinavyotoa mafunzo ya kilimo vyahimizwa kuwa na kozi fupi za masomo kunoa zaidi wanafunzi, mbali na taaluma wanazosomea

Na SAMMY WAWERU

VYUO vinavyotoa mafunzo ya kilimo vimehimizwa kuwa na kozi zinazochukua muda mfupi, mbali na taaluma ambazo wanafunzi wanasomea.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya pembejeo ya Elgon Kenya, Dkt Bimal Kantaria amesema kozi hizo zishirikishe shughuli zinazotekelezwa nyanjani – shambani.

Dkt Kantaria alisema mafunzo hayo yatasaidia kuwezesha wanafunzi kuelewa kwa kina yanayohijika shambani.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuboresha kwa kiasi kikubwa sekta ya kilimo na ufugaji nchini.

“Ni muhimu vyuo viwe na kozi zingine za pembeni, zinazochukua muda mfupi kunoa wanafunzi kando na taaluma wanazosomea,” akasema afisa huyo akizungumza jijini Nairobi.

“Sekta ya kilimo itakuwa kwa kiwango kikubwa hatua mahususi zikichukuliwa, kuanzia vyuoni.”

Elgon Kenya ni tajika Ukanda wa Afrika Mashariki katika utengenezaji na usambazaji wa fatalaiza, mbegu na dawa dhidi ya magonjwa na wadudu waharibifu shambani.

Kauli ya Dkt Kantaria imejiri miezi michache baada ya Idara ya Masuala ya Vijana kuelezea wasiwasi kuhusu mtazamo wa vijana katika sekta ya kilimo na ufugaji.

Julai mwaka huu, Katibu katika idara hiyo, Bw Charles alisema idadi ya vijana wanaoendeleza kilimo ni ya chini mno.

Bw Sunkuli aidha alieleza kusikitishwa kwake na mtazamo wa vijana na jamii katika sekta ya kilimo.

“Tumeona baadhi ya wataalamu wakigura sekta ya kilimo na ufugaji. Ni jambo la kushangaza, na linaibua maswali chungu nzima kuhusu maisha ya usoni ya sekta hii ambayo ni nguzo ya uchumi wa taifa,” akasema.

Katibu huyo alitumia mfano wa taasisi zinazotoa mafunzo ya kilimo nchini, idadi ya wanafunzi wanaochagua kozi za kilimo akiitaja kuwa ya chini sana.

“Wanaofuzu, hawataki kuvalia ovaroli na gambuti na kuenda shambani. Wanataka ajira wanazoketi kwenye kompyuta,” akaelezea.

“Tunahitaji kutathmini mfumo wetu wa elimu, usiwe ule wa kusomesha vijana kutegemea kazi za ofisi pekee. Ujumuishe kazi za nyanjani,” Bw Sunkuli akapendekeza.

Elgon Kenya ni miongoni mwa kampuni zinazotoa huduma za kilimo nchini, na ambayo Wizara ya Kilimo imetambua kutokana na mchango wake mkuu na hata kuituza kufuatia jitihada kuboresha sekta ya kilimo Kenya na Afrika Mashariki kwa jumla.

You can share this post!

Mufya yatwaa taji la Patrick Oboya Cup

Marionex: Uvumilivu ndio siri ya mafanikio ya mambo mengi

T L