• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 6:55 PM
Wa Iria achemka kuambiwa Raila ‘hatakikani’ Murang’a

Wa Iria achemka kuambiwa Raila ‘hatakikani’ Murang’a

NA LAWRENCE ONGARO

ALIYEKUWA Gavana wa Murang’a Bw Mwangi Wa Iria amesema viongozi wa Mlima Kenya wanastahili kujitokeza wazi na kutetea haki ya wananchi bila kuwa na shaka.

Aliyasema hayo baada ya juhudi zake za kutaka kibali kuandaa mkutano wa kisiasa Murang’a leo Ahamisi kugonga mwamba.

Afisa mkuu wa polisi wa Murang’a David Mathew alisema mkutano wa Azimio wa kutaka kuzungumza na wananchi hautakubaliwa.

Na sasa Wa Iria amesema ataanza ziara ya kuzunguka kaunti ya Murang’a ili kutetea haki ya wananchi na kusikiliza maoni yao.

“Iwapo tutazuiliwa na polisi kufanya mikutano yetu na wananchi, tutajua ya kwamba serikali haitaki mwananchi apate haki yake,” alisema Bw Wa Iria.

Alisema katika maeneo mengine ya nchi kama Ukambani, Mombasa na hata Kisumu, viongozi hukutana bila kuzuiliwa na yeyote lakini ikifika mikutano ya Mlima Kenya kunatokea shida.

Bw Wa Iria alitoa maoni hayo mjini Thika mnamo Jumatano, baada ya kunyimwa kibali cha mkutano mjini Murang’a.

Alipanga kuwakaribisha viongozi wa Azimio mjini Murang’a ili kujadiliana na wananchi kuhusu shida zao.

Alisema kulingana na uchunguzi wake viongozi wengi wa Mlima Kenya wameshindwa kutetea wananchi ili kupata maoni yao.

Alisema mkutano wowote ukitibuka hawatarudi nyuma bali wataendeleza harakati za kutafuta maoni ya wananchi.

Bw Wa Iria alisema atajitokeza wazi kutetea jamii ya Mlima Kenya ili kuikomboa ili iweze kuwa huru na kupata haki.

Anapanga kuzuru maeneo ya Mlima Kenya kama Kiambu, Nyeri na hata Murang’a ili kujadiliana na wananchi maswala muhimu yanayowakumba.

Alisema kila Mkenya ana haki ya kupata haki yake badala ya watu wachache.

“Mimi kama mzaliwa wa Mlima Kenya nitaendelea kutetea jamii yetu hadi mwisho,” aliahidi.

Alisema iwapo mambo yataendelea hivyo bila shaka hata mikutano kama ya chamaa au vyama vya wanawake itaanza kuzimwa “hasa hapa Mlima Kenya.”

  • Tags

You can share this post!

Mkulima Wangari Kuria ambaye amejizolea lakabu...

Viongozi wa dini ya Kiislamu wataka waumini kusubiri...

T L