• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Wabunge wamwidhinisha mke wa Chebukati kuwa Mwenyekiti wa CRA

Wabunge wamwidhinisha mke wa Chebukati kuwa Mwenyekiti wa CRA

NA CHARLES WASONGA

MKEWE aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati, Mary Wanyonyi, ameidhinishwa rasmi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA).

Mnamo Alhamisi, wabunge waliunga mkono ripoti ya Kamati ya Fedha na Mipango iliyopendekeza kuwa Bw Wanyonyi amehitimu na kufaa kwa wadhifa huo.

Kamati inayoongozwa na Mbunge wa Molo Kuria Kimani, ilimpiga msasa Bi Wanyonyi mnamo Juni 22, 2023.

“Baada ya kumhoji na kukagua stakabadhi zake za masomo, kamati hii imefikia uamuzi wa pamoja kwamba Bi Wanyonyi amehitimu kwa wadhifa wa Mwenyekiti wa Tume ya Ugavi wa Rasilimali (CRA),” Bw Kimani akasema alipowasilisha rasmi ripoti hiyo.

Rais William Ruto alimteua Bi Wanyonyi kwa wadhifa huo kuchukua nafasi ya Dkt Jane Kiringai, aliyestaafu baada ya kukamilisha muhula wake wa miaka sita.

Kulingana na katiba ya sasa, mshikilizi wa cheo hicho atahudumu kwa kipindi kimoja kwa miaka sita ambacho hakiwezi kuongezwa.

Bi Wanyonyi sasa atahudumu kwa kipindi hicho, cha miaka sita, kama mkuu wa tume hiyo ambayo hupendekeza kiwango cha ugavi wa mapato kati ya Serikali Kuu na serikali za kaunti.

Aidha, tume hiyo pia huamua mfumo wa ugavi wa mapato baina ya serikali zote 47 za kaunti.

Baada ya kuidhinishwa na Bunge, sasa Rais atamteua rasmi Bi Wanyonyi kisha alishwe kiapo kabla ya kuanza kuchapa kazi rasmi.

  • Tags

You can share this post!

Korti yazima kesi iliyosukumwa na kampuni ya Gachagua...

Madereva wa masafa marefu kugomea agizo wasome upya

T L