• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Korti yazima kesi iliyosukumwa na kampuni ya Gachagua kutaka wakili na mteja washtakiwe

Korti yazima kesi iliyosukumwa na kampuni ya Gachagua kutaka wakili na mteja washtakiwe

NA RICHARD MUNGUTI

JITIHADA za kampuni ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kumshtaki wakili na mteja wake wanayeng’ang’ania umiliki wa shamba la Sh1.5 bilioni zimegonga mwamba baada ya Mahakama Kuu kumzima Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuendelea na kesi aliyowafungulia.

Jaji Mugure Thande alisimamisha kushtakiwa kwa Moses Owuor (wakili) na Bw John Michael Otieno Ohas hadi kesi waliyowasilisha katika Mahakama Kuu isikilizwe na kuamuliwa.

Jaji Thande aliorodhesha kesi hiyo kutajwa Oktoba 11, 2023 kwa maagizo zaidi.

Chama cha mawakili nchini (LSK) na Bw Owuor kiliwasilisha kesi kupinga hatua ya DPP kumshtaki wakili huyo kutokana na kazi yake.

Kupitia kwa rais wa LSK Eric Theuri, Jaji Thande alifahamishwa kwamba Owuor alikamatwa siku mbili kabla ya Bw Gachagua kufika katika Mahakama Kuu mnamo Juni 21/22, 2023 kutoa ushahidi kuhusu umiliki wa shamba hilo la hekta mbili linalong’ang’aniwa na kampuni yake (Naibu Rais) kwa jina Wamunyoro Investment Limited na kampuni ya Ohas kwa jina Columbus Two Thousand Limited.

Mnamo Juni 16, 2023, Ohas alifikishwa kortini na kuzuiliwa katika seli za mahakama ya Milimani.

Owuor alienda kumwona Ohas kisha akatiwa mbaroni na wote wakafikishwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Lucas Onyina kujibu mashtaka ya kula njama kulaghai kampuni ya Wamunyoro shamba la hekta mbili la thamani ya Sh1.5 bilioni.

Jaji Thande aliombwa asitishe kukamatwa na kushtakiwa kwa Bw Owuor mbele ya Onyina.

Bw Theuri na wakili Apollo Mboya wanaomwakilisha Owuor walimkabidhi Bw Onyina agizo la Mahakama Kuu kisha akasimamisha kesi hiyo hadi Mahakama Kuu itakapoamua kesi ya kupinga kushtakiwa kwa wawili hao kutokana na kesi hiyo ya umiliki wa shamba.

Bw Gachagua anayewakilishwa na Philip Nyachoti hakufika katika Mahakama Kuu kwa sababu za kazi.

  • Tags

You can share this post!

Mourinho apigwa marufuku ya siku 10 na kutozwa faini ya...

Wabunge wamwidhinisha mke wa Chebukati kuwa Mwenyekiti wa...

T L