• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Wachungaji kutoka Thika Mashariki watakasa eneo la mauti

Wachungaji kutoka Thika Mashariki watakasa eneo la mauti

Na LAWRENCE ONGARO

VIONGOZI wa makanisa manane na waumini walikongamana kwenye eneo la mauti katika kijiji cha Gatuanyaga, Kaunti ya Kiambu, na kufanya maombi yaliyochukua muda wa saa tatu.

Mwezi mmoja uliopita, watu kadha waliuawa kinyama katika eneo hilo. Na ndiyo sababu ya wachungaji hao kufika hapo Jumapili kwa utakaso na maombi ili kufukuza pepo wachafu.

Wakiongozwa na Askofu mkuu wa kipentekosti mjini Thika, Bw Kennedy Mbatia, wachungaji hao walilaani unyama huo ambapo watu wasio na hatia waliuawa kiholela na baadaye miili yao ikatupwa katika msitu mmoja eneo la Gatuanyaga, Thika Mashariki.

“Sisi kama wachungaji tumefika hapa tukiamini watu wale waliohusika na kitendo hicho watapata hukumu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo bado hawajaepuka kichapo cha Mungu,” alifafanua Askofu Mbatia.

Alisema katika eneo hilo la Thika Mashariki, wachungaji wamekubaliana ya kwamba viongozi wa kisiasa watakaofika kanisani hawatapewa nafasi kusimama mbele ya madhabahu kupiga siasa walizozitaja ni za chuki.

“Hata hivyo, viongozi hao watapewa nafasi kuzungumza nje ya makanisa ili kuongea na wananchi,” alifafanua Askofu huyo.

Aliwashauri viongozi popote walipo wawe na unyenyekevu wanapohutubia wananchi kwa sababu “sote tunatarajia kuwa na uchaguzi wa amani ifikapo mwaka ujao wa 2022.”

Waliiomba serikali kuwa macho ili kuzuia viongozi wanaeneza chuki na uhasama hasa wakitaka amani irejeshwe kabisa eneo la Laikipia.

Wachungaji hao waliwahimiza Wakenya popote walipo wazingatie maombi na wazingatie amani ili tunapokwenda uchaguzini tuwe kitu kimoja.

  • Tags

You can share this post!

Haaland abeba Borussia Dortmund dhidi ya Union Berlin ligini

Matokeo mseto Kenya ikianza ndondi za majeshi nchini Urusi