• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Wachuuzi Londiani warejea barabarani licha ya ajali iliyoangamiza 52

Wachuuzi Londiani warejea barabarani licha ya ajali iliyoangamiza 52

NA MERCY KOSKEI

HALI ya kawaida imeanza kurejelea katika makutano ya Londiani, barabara kuu ya Kericho-Kisumu siku mbili baada ya ajali mbaya iliyosababisha maafa ya watu 52 na wengine 31 kuuguza majeraha kufanyika.

Mnamo Jumamosi, Julai 1, 2023 wafanyabiashara hawakufungia maduka, ambapo madereva wa lori na matrela hutegemea kununua bidhaa.

Hata hivyo, Jumapili Taifa Leo Digitali ilipozuru eneo hilo biashara kwenye soko linalotumika kama kituo kikuu cha ununuzi na wakaazi wa Londiani, Chepseon, na Kedawa Kaunti Ndogo ya Kipkelion kazi iliendelezwa kama kawaidwa.

Wafanyabiashara ambao vibanda vyao viliharibiwa, walikuwa wakijishughulisha na kuokota vipande vilivyovunjwa na kuweka makazi ya muda ya biashara zao na kuendelea na shughuli zao za kila siku.

Amos Korir, mfanyibiashara, alisema kuwa wakati wa ajali hiyo alikuwa akimhudumia mteja na punde aliskia kishindo kikubwa na baadaye mayowe.

Alisema kuwa ana bahati kwani ajali hiyo ilitokea upande wa pili wa barabara lakini rafiki yake mwendesha bodaboda hakubahatika kwani aliangamia.

Baba huyo wa watoto watatu alisema, ilimbidi arejelee kazini ambapo amekuwa akifanya biashara ya kuuza nyanya na matunda kwa zaidi ya miaka kumi na mitano ili kutunza familia yake.

Wachuuzi eneo la Londiani, kandokando mwa barabara kuu ya Kericho-Kisumu waendeleza biashara kama kawaida licha ya ajali mbaya. Picha|BONFACE MWANGI

Akiwa hana njia nyingine ya kujikimu kimaisha, Bw Korir alisema kwamba alilazimika kurejea ili kujaribu bahati yake.

“Tunaomboleza msiba wa wafanyabiashara wenzetu lakini cha kusikitisha ni lazima tuendelee na biashara zetu. Tuna familia zinazotutegemea. Ninauza nyanya ambazo zinaweza kuharibika nilizonunua Alhamisi jioni, na nilipaswa kuhakikisha kuwa zimeisha kufikia leo (Jumapili),” akasema mchuuzi huyo.

Bi Mercy Kerubo, anayeuza viazi, nyanya, na vitunguu alisema kuwa ajali hiyo iliwaacha wakazi katika mshangao na maombolezo kufuatia nafsi zilizoangamia.

Kulingana na Bi Kerubo, wakati wa kisa hicho alikuwa ameondoka kuelekea nyumbani baada ya jirani yake kumpigia simu na kumjulisha kuwa bintiye alikuwa ameugua.

Alisema, kwa bahati mbaya, wafanyabiashara walisusia kufika kazini lakini kwa sababu hawana njia nyingine ya kujipatia riziki wamelazimika kurejea.

Hata hivyo, alisema kuwa hatua ya serikali kuhamisha biashara zao itawaathiri kwani wanategemea madereva na wasafiri wanaotumia barabara hiyo kuu.

“Tumeambiwa tutoke barabara tuhamishe biashara zetu sokoni umbali wa kilomita kadhaa. Tunategemea madereva na wasafiri wanaotumia barabara hii, na wengi wataendelea na safari hasa kwa kuwa bei ya mafuta imepanda hivyo basi hawatafika sokoni. Ninahofia kuwa biashara zetu zitashuka,” alisema.

Waziri wa Uchukuzi Bw Kipchumba Murkomen siku ya Jumamosi, alifichua kuwa serikali inapanga kuwahamisha wachuuzi wanaofanya biashara kandokando mwa barabara kuu nchini.

Ajali hiyo ya Juni 30, 2023 ilihusisha lori lililokuwa likitoka Nakuru likielekea Kericho ambapo lilipoteza mwelekeo na kugonga matatu, magari ya kibinafsi, pikipiki na wachuuzi.

 

  • Tags

You can share this post!

Msanii Mike Rùa adai atakutangulia ufalme wa Mbinguni 

Tanzia, Shatta Bwoy akimuaga mkewe kwa kuwekelea nywele...

T L