• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Msanii Mike Rùa adai atakutangulia ufalme wa Mbinguni 

Msanii Mike Rùa adai atakutangulia ufalme wa Mbinguni 

NA MWANGI MUIRURI

MWIMBAJI wa Mugithi kutoka eneo la Mlima Kenya mwenye sifa ya kuwa na ulimi mchafu zaidi, Mike Rùa sasa anasema atakutangulia kurithi ufalme wa mbinguni.

Katika maisha ya watu wa Mlima Kenya, kanda zilizo na nyimbo za msanii huyu hufichwa hata kuliko mihadarati kwa kuwa hata ikiwa zinapendwa si haba, sio za kusikilizwa ovyoovyo bila kuzingatia nidhamu ndani ya maadili ya kimsingi.

Hata baadhi ya mapasta hupenda nyimbo zake lakini huzicheza kwa sauti ya chini, sanasana ndani ya gari la kibinafsi milango na madirisha yakiwa yamefungwa.

Bw Rùa anasema raha yake kuu akiwa katika jukwaa la burudani ni “kuwaona mkichachawika kiasi cha kulia mkinengua kiuno huku nduru zikitanda wakati nakazana kuwaroga na maneno mazito mazito na makali kiasi cha kuogofya”.

Na sio eti ataokoka na kukiri imani kuwa Mwokozi wa maisha yake, bali anasema uwazi wake na kusaka kukufurahisha kupitia nyimbo hizo ndio pasipoti yake ya kuingia mbinguni.

Rùa ambaye kwa sasa yuko ndani ya miaka 50 katika uhai wake, anafahamika vyema kupitia nyimbo zake chafuchafu ambapo huporomosha maneno ya ngono, viungo vya mwili na pia tabia zote mbaya bila kujali.

Nyimbo zake nyingi haziwezi zikachezwa katika vyombo vya habari na hata katika sekta ya burudani kulikojaa walevi, nyimbo hizo huanza kuchezwa usiku wa manane–yale masaa ya wezi, wachawi na polisi.

“Lakini mbona mwanihukumu na vile wengi hata mapasta wananipenda? Mimi ni muwazi na hucheza ngoma ambazo mashabiki wangu wamelilia. Wewe na uokovu wako una shida. Sisi hapa katika mtindo na mbinu zetu tuko sawa,” akaambia Taifa Leo Dijitali.

Bw Rùa alisema: “Mimi katika utunzi wa ngoma zangu hutumia lugha yetu tamu ya Gikuyu na maneno yote ambayo husikika nikitumia yako kwenye kamusi yetu ya kijamii”.

Alielezea, kile tu mimi hufanya ni kujivunia lugha yangu kiasi cha kuyatumia maneno ambayo mnajifanya hayako na mngetaka yasahaulike.

Ni mtindo wa kipekee ambao hakuna chipukizi wa usanii anayeonekana kuthubutu kumuiga kiasi kwamba hofu imetanda miongoni mwa mashabiki wake kwamba akiondoka kutoka ulingo wa burudani, mtindo huu wake utaisha.

“Ningetaka kuwasihi mjizatiti na muige mtindo huu wangu kwa kuwa ni wa kipekee, huhitaji ubunifu wa hali ya juu, hauna ushindani mkali na una pesa…Msifanye mtindo huu wangu upotee,” akasema Bw Rùa.

 

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Maajabu Meya Mexico akioa mamba

Wachuuzi Londiani warejea barabarani licha ya ajali...

T L