• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Wachuuzi walivyovuna kufuatia msongamano wa magari msimu wa Krismasi

Wachuuzi walivyovuna kufuatia msongamano wa magari msimu wa Krismasi

NA RICHARD MAOSI

WACHUUZI katika barabara ya Nairobi-Nakuru walivuna pakubwa kufuatia msongamano mkubwa wa magari ulioshuhudiwa kabla na wakati wa msimu wa Krismasi, wanaoishi mijini walipokuwa wakielekea mashambani.

Biashara ya vyakula, vinywaji na matunda zilinoga katika maeneo ya Kimende, Kijabe, Flyover na Weighbridge.

Aidha bei ya bidhaa ilipanda zaidi ya maradufu wafanyibiashara waking’ang’ania wateja.

Kwa upande mwingine, matapeli walipata mwanya kuuzia wasafiri bidhaa ghushi ambazo hazijaafikia ubora.

Katika mahojiano na Taifa Leo Dijitali, Ali Noor ambaye ni mchuuzi wa maji, biskuti, soda na maziwa anasema kinyume na mwaka uliopita, 2022, wasafiri wengi 2023 walielekea vijijini kufurahia Krismasi na familia zao.

Kulingana na Ali, lita moja ya maji ilikuwa inauzwa Sh80, ikiwa ni ongezeko la Sh30.

Soda pia ilipanda kutoka Sh60 hadi Sh90.

Alisema mazingira ya kufanya biashara yaligeuka kuwa mazuri, kinyume na miezi kadhaa iliyopita ambapo wachuuzi walikuwa wakihatarisha maisha yao kwa kukimbizana na magari.

Kwa siku tatu, mfululizo – kuanzia Desemba 24 hadi 26, Ali alisema alitengeneza hela nzuri na angependa hali kama hiyo iendelee angalau mpaka mwanzoni mwa 2024.

“Ingawa uchumi imetubana, ni furaha isiyo kifani kuwa na pesa mfukoni,” akasema.

Irene Akoth mkaazi wa Nairobi alisema alikuwa akisafiri kuelekea Naivasha kuponda raha wikendi iliyopita, lakini akajikuta katikati ya msongamano wa magari.

Alitumia njia ya Maai Mahiu baada ya magari kukwama kilomita chache kutoka Rironi.

Akoth alisema alipokuwa safarini, alikula na akashiba, ndiposa anawapongeza wachuuzi wa vyakula rejareja akisema 2023 walijipanga vilivyo.

Aliondoka Nairobi Ijumaa japo alifika Naivasha Jumamosi, Desemba Desemba 23 baada ya gari lake kukwamia eneo la Longonot.

Ijumaa, Waziri wa Babara na Uchukuzi, Bw Kipchumba Murkomen alihimiza madereva kuchukua tahadhari ili kuepuka ajali za mara kwa mara wanaposafirisha watu.

Aidha, wamiliki wa magari ya masafa marefu umma walitakiwa kuwa na madereva wawili ili kutoa kuwapa muda wa kutosha kupumzika.

  • Tags

You can share this post!

Krimasi: Washukiwa 34 wa uhalifu wakamatwa Starehe

Dorice Aburi: Nilikuwa ninajizungumzia

T L