• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:50 AM
Krimasi: Washukiwa 34 wa uhalifu wakamatwa Starehe

Krimasi: Washukiwa 34 wa uhalifu wakamatwa Starehe

NA SAMMY KIMATU

WASHUKIWA 34 wa uhalifu walikamatwa usiku wa kuamkia Jumatano, Desemba 27, 2023 katika Kaunti Ndogo ya Starehe, Nairobi kufuatia oparesheni iliyoendeshwa kukabiliana na visa vya uhuni msimu wa Krismasi.

Msako huo ulihusisha asasi mbalimbali za serikali, wakiwemo machifu na maafisa wa polisi wanaoimarisha ulinzi katika kituo cha Shirika la Reli Nchini (KRC), Jijini Nairobi.

Aidha, oparesheni hiyo ya mtaa wa Railways iliongozwa na chifu wa eneo la Landi Mawe, Bw Geoffrey Maina.

Msako huo ulilenga wezi wa simu, wanaopora watu pesa, na waliokiuka kanuni za unywaji pombe.

Baadhi ya askari na machifu waliofanya msako kukamata wahalifu eneo la Starehe, Nairobi msimu wa Krismasi 2023. PICHA|SAMMY KIMATU

Hali kadhalika, wanaouza dawa za kulevya na mihadarati walijipata kuandamwa na mkono wa sheria.

Akithibitisha kukamatwa kwa washukiwa hao wa uhalifu, Naibu Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Starehe, Bw Dennis Omuko alisema kati 34 waliotiwa pingu, 12 walikuwa raia wa Burundi.

“Operesheni hiyo ililenga kukabiliana na visa vya uhalifu katika mitaa yetu wakati wa sherehe za Krismasi, Mwaka Mpya na baada ya msimu wa sherehe,” Bw Omuko aliambia Taifa Leo Dijitali.

Afisa huyo alibainisha kwamba washukiwa waliokamatwa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Industrial Area, ili kuruhusu uchunguzi kufanyika, ikiwemo kuhojiwa, kabla kufikishwa kortini.

 

  • Tags

You can share this post!

Sudi adai yeye ndiye ‘mpishi’ katika serikali...

Wachuuzi walivyovuna kufuatia msongamano wa magari msimu wa...

T L