• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:44 PM
Wafanyakazi 7,000 wahofia ajira zao serikali ikibinafsisha bandari

Wafanyakazi 7,000 wahofia ajira zao serikali ikibinafsisha bandari

Na ANTHONY KITIMO

WAFANYAKAZI zaidi ya 7,000 wanaofanya kazi katika Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA) huenda wakapoteza kazi yao.

Wafanyakazi hao wana wasiwasi huku kampuni za kibinafsi zikilenga mabilioni ya pesa kutokana na mpango wa ubinafsishaji unaotarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Huku sekta ya kibinafsi ikitarajiwa kumiliki takriban mali tisa za KPA baada ya kukamilika kwa mchakato wa ubinafsishaji kabla ya mwisho wa mwaka huu, wafanyakazi hao sasa hawajui hatima yao.

“Tunashangaa jinsi viongozi wetu na hata chama cha kutetea maslahi yetuv cha maakuli (DWU) ambao wamekuwa katika mstari wa mbele kulinda haki zetu walivyokimya. Tumesubiri watoe msimamo wao kuhusu suala hilo lakini hakuna mawasiliano,” alisema mfanyakazi mmoja wa KPA.

Serikali ya Kenya Kwanza, inanuia kukodisha bandari zake muhimu kwa lengo la kuimarisha ushindani katika sekta ya baharini kukusanya angalau Sh1.4 trilioni kila mwaka ifikapo 2030.

Wiki hii, KPA ilitoa zabuni za kukodisha sehemu ya vituo vya bandari za Mombasa na Lamu kwa wahudumu wa kibinafsi huku mfumo wa usimamizi wa bandari ukitarajiwa kufanyika katika kile kinacholenga kufanya ukanda wa Kaskazini kuwa wenye ushindani.

Kulingana na mpango wa Rais William Ruto, utawala wake unatafuta wawekezaji wa kibinafsi kuchukua utendakazi na usimamizi wa vituo vitano muhimu vya bandari zikiwemo bandari za Mombasa na Lamu, Maeneo Maalum ya Kiuchumi ya Dongo Kundu, bandari ya Kisumu na bandari ya Shimoni kwa wawekezaji kupitia ushirikiano.

Rais Ruto alisema hatua hiyo itavifanya vituo vya bandari ambavyo vimekuwa vikikabiliwa na changamoto ya msongamano kuwa na ushindani.

Wiki hii, Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA) ilianza mchakato wa kukodisha mali tisa za bandari; chini zabuni nambari KPA/052/2023-2024/CPS. Wenye nia ya kushiriki wana hadi Oktoba 12 kuwasilisha maombi yao.

“Zabuni zilizokamilika itawasilishwa kabla ya tarehe 12 Oktoba 2023,” ilisema taarifa kwa umma chini ya mkurugenzi mkuu wa KPA Kapteni William Ruto.

Kulingana na KPA, wawekezaji kutoka taasisi za kibinafsi wanaalikwa kutoa zabuni kama kampuni binafsi au kupitia Ubia.

Katibu Mkuu wa DWU Simon Sang aliahidi kutoa mwelekeo wake hivi karibuni.

“Tumekutana na KPA na kupata habari zaidi kuhusu mchakato mzima na hivi karibuni tutatoa msimamo wetu kuhusu hilo,” alisema Bw Sang.

Katibu huyo amekuwa akipinga ubinafsishaji wa vituo vya KPA lakini kimya chake kimeleta shaka miongoni mwa wafanyikazi.

“Tunashuku chama cha wafanyakazi hakitakuwa upande wetu wakati huu kwani tunahofia huenda tukapoteza kazi yetu,” akasema mmoja wa wafanyakazi.

  • Tags

You can share this post!

El Nino itasababisha njaa kubwa, walia wakazi wa Maya

Wakazi wa Taita Taveta wataka Ruto atimize ahadi alizowapa

T L