• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Waislamu wakashifu kitabu chenye mchoro wa Mtume unaotaka wanafunzi wapake rangi

Waislamu wakashifu kitabu chenye mchoro wa Mtume unaotaka wanafunzi wapake rangi

NA WINNIE ATIENO

WAUMINI wa dini ya Kiislamu wamekashifu vikali mchapishaji vitabu kwa kuchapisha kitabu chenye mchoro uliosemekana kitabuni kuwa ni wa kuashiria Mtume Muhammad.

Kwenye kitabu hicho cha Grade 2 Mentor Encyclopedia, kampuni ya uchapishaji vitabu ya Mentor Publishing Co LTD ilichora picha hiyo ikitaka wanafunzi wa somo la dini ya Kiislamu (IRE) kuupaka rangi mchoro huo.

Hata hivyo, waumini wa dini hiyo na viongozi wa kidini walishtumu hatua hiyo wakisema ni kukufuru.

Aidha, waliitaka Wizara ya Elimu kumchukulia hatua za kisheria mchapishaji huyo ambaye baadaye aliomba radhi.

“Mtoto wangu alikuwa anafanya masomo yake ya ziada kama kawaida yake nikaona akipaka rangi picha ya Mtume Muhammad, nilishtuka kuona kufuru. Walidhamiria nini kuchapisha picha hiyo?” aliuliza Bw Galgalo Gurre, mzazi katika Kaunti ya Mombasa.

Mzazi mwingine, Bi Amina Mohammed alishangaa endapo serikali inasimamia machapisho ya vitabu vya watoto wanavyotumia shuleni.

“Nani anawaangalia ama wanaweza kuchapisha chochote wanachokitaka? Kama Muislamu nimeshangaa sana, haya ni makosa makubwa sana,” alisema Bi Mohammed.

Hata hivyo, mchapishaji huyo aliomba msahama na kulazimika kuagiza vitabu vyote kwenye soko viregeshwe.

“Tulichapisha mchoro kuashiria Mtume Muhammed kimakosa kitabu cha wanafunzi. Tunaomba msamaha na kuahidi kutorudia kosa hilo tena. Tumechukua mikakati kabambe kurekebisha kosa letu na kuhakikisha haturudii kosa hilo tena,” Mkurugenzi Mkuu wa Mentor Publishing Co Ltd, Bi Josephine Wanjuki, akasema.

“Tumegundua makosa tuliyofanya kwenye uchapishaji wa kitabu chetu cha Mentor Encyclopedia Grade 2. Tunawaomba msahama na tumeanza ushirikiano na Baraza la Kiislamu la Elimu, Msikiti wa Jamia huko Nairobi, Masjid Al Ameen na washikadau wengine,” akaongeza Bi Wanjuki.

Bi Wanjuki alisema kampuni hiyo imechukua hatua madhubiti ikiwemo kuondoa vitabu vyenye uchapishaji huo kutoka katika soko.

“Vilevile, tumeondoa picha hiyo kwenye vitabu ambavyo tulipania kuchapisha na hatua ya kutathmini vitabu vyote vya IRE tukishirikiana na Baraza la Kislamu la Elimu kabla ya kuchapisha,” Bi Wanjuki alisema.

Vitabu vyote vilivyo na mchoro huo uliozua malalamishi vimeanza kuondolewa kwenye soko.

“Vitabu vya Mentor Encyclopedia Grade 2 vilivyoko kwenye stoo havitapelekwa sokoni, vile viko kwenye maduka ya wauzaji vitabu na mitaani vimeanza kurejeshwa kwa mchapishaji,” alisisitiza.

Aliwasihi walimu, wanafunzi, wasimamizi wa shule za msingi na yeyote mwenye kitabu hicho kukikabidhi katika maktaba ya msikiti wa Jamia, Al-Ameen na Baraza la Kislamu la Elimu.

“Tunahakikishia jamii ya Kiislamu ushirikiano wetu nao ili tusirudie kosa hili tena,” alisisitiza.

  • Tags

You can share this post!

AKILIMALI: Huuzia wagonjwa maji moto kujipatia riziki

Mgogoro Meru: Wapinzani wa Mwangaza sasa wageukiana

T L