• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Wakazi wa Kiambu wahimizwa kuendea chanjo ya corona

Wakazi wa Kiambu wahimizwa kuendea chanjo ya corona

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Kaunti ya Kiambu wamehimizwa kujitokeza kwa wingi ili waendelee kuchanjwa dhidi ya homa ya Covid-19.

Waziri wa afya wa kaunti hiyo Dkt Joseph Murega, aliwashauri vijana kujitokeza kwa wingi kuhakikisha wamechanjwa.

Alieleza kuwa tayari watu 500,000 wamechanjwa Kaunti ya Kiambu, ambapo wanatarajia wale hawajapokea chanjo hiyo watajitokeza kwa wingi kabla ya mwezi Disemba 2021, kukamilika.

“Chanjo zote ziko sawa kwa hivyo hakuna haja ya kuchagua. Cha muhimu kwa wakati huu ni kupata kinga ya chanjo hiyo mwilini,” alifafanua Dkt Murega.

Aliyasema hayo eneo la Juja wakati wa kuhamasisha wakazi juu ya umuhimu wa chanjo dhidi ya Covid-19.

Alieleza kuwa dozi za chanjo ziko kwa wingi ambapo wameweka mikakati ya kuchanja watu katika maeneo ya umma.

Alitaja maeneo hayo kama vituo vya magari, sokoni, na kituo cha polisi.

Alisema wanafanya hivyo kutoka saa 9 za mchana hadi saa 3 za usiku.

Alieleza kuwa tangu wakazi wa Kiambu kujitokeza kwa wingi kwa chanjo hiyo miezi saba iliyopita virusi vya corona vimepungua kwa kiwango kikubwa.

Alitoa wito kwa vijana hasa wa hadi umri wa miaka 24 kujitokeza kwa wingi ili kupata chanjo hiyo.

Wengi wa akina dada waliohudhuria hafla hiyo walipokea sodo na sabuni kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Kiambu, na mashirika mengine.

“Vijana ndio wanajumuika na wenzao mara nyingi na kwa hivyo ni vyema kujichunga kwa kupokea chanjo hiyo,” alifafanua Dkt Murega.

Alisema kaunti ya Kiambu kwa wakati huu ina dozi za kutosha ambapo ifikapo mwisho wa mwezi Disemba wangetaka kuona watu zaidi ya 800,000 wakiwa wamechanjwa.

Hata hivyo aliwaonya wakazi hao wawe makini kutokana na vitisho vipya vya kirusi kipya kwa jina Omicron ambacho ni hatari.

“Kwa hivyo, kwa wakati huu ni vizuri kupata kinga mwilini ili kujizuia dhidi ya maambukizi yanayoweza kutokea,” alifafanua Dkt Murega.

You can share this post!

Omanyala sasa ni Inspekta wa Polisi, atawakilisha idara...

Ashtakiwa kwa kuiba Biblia

T L