• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Wakazi wa Molo wachoma maskani ya chang’aa wakiilaumu kwa maafa ya vijana

Wakazi wa Molo wachoma maskani ya chang’aa wakiilaumu kwa maafa ya vijana

NA JOHN NJOROGE

Takriban nyumba nne zimeteketezwa na wakazi wenye hasira katika kijiji cha Chandera,Turi, Molo Kaunti ya Nakuru, Jumatano Novemba 15, 2023 jioni.

Wakazi hao walioandamana na kubeba matawi kwenye barabara ya Turi-Chandera, walivamia baadhi ya nyumba ambazo walidai pombe hiyo inauzwa na kuzichoma moto huku wakishutumu uongozi kwa ulegevu wa kusitisha uuzaji unaoendelea ambao umesababisha vifo vya vijana katika eneo hilo.

Taifa Leo ilipofika eneo la tukio, wakazi walikuwa wakivunja kutoka nyumba moja hadi nyingine ambako uuzaji huo unafanyika, na kuziteketeza moto.

Wakazi katika eneo walilosema pombe haramu huuzwa katika kijiji cha Chandera, Molo katika Kaunti ya Nakuru mnamo Novemba 15, 2023.
Picha|John Njoroge

“Tumesema imetosha. Hatutaruhusu kijana yeyote kupoteza maisha yake kutokana na pombe haramu ambayo inauzwa kwa wingi eneo hili,” alisema Bi Margaret Wambui, mkazi.

Alisema kuwa watoto wameachwa bila wazazi huku wake wakiwa wajane kufuatia pombe hiyo katika eneo hilo.

Wakazi hao walilaumu wasimamizi wa eneo hilo ambao waliwashutumu kwa kuchukua hongo kutoka kwa wauzaji.

“Tunamwomba Naibu Rais Rigathi Gachagua atembelee eneo letu na atuepushe na uuzaji huu usiokoma wa pombe ya kizazi cha pili kwani hatutaki kushuhudia vifo vingi kutoka kwa watu wasio na hatia,” akasema Bi Mary Njeri, mkazi.

Kina mama walio na uchungu wa kupoteza wana wao na wake wa waume ambao wamekufa kwa kunywa pombe hiyo, walipiga kelele na kuomboleza wakati wa zoezi zima.

Baada ya kubaini kuwa wananchi walikuwa na hasira, Chifu wa eneo hilo alijiunga na kuwaongoza wakazi hao hadi kwenye eneo la mauzo hayo.

Polisi waliofika eneo la tukio saa chache baadaye, walilazimika kufyatua vitoa machozi kwa umati wa watu waliokuwa wakiendelea kuchoma nyumba hizo lakini hilo halikuwazuia kwani tayari walikuwa wamekamilisha azma yao ya kuchoma maskani ya chang’aa.

Tukio hilo limetokea saa chache baada mmoja wa mkazi anayeshukiwa kufariki kutokana na pombe hiyo, alizikwa.

Kulingana na wakazi, takriban watu watatu wamekufa katika muda wa wiki moja kutokana na pombe hiyo haramu.

Jumatatu asubuhi, maafisa wa polisi waliokuwa wakiwasindikiza wasimamizi wa vituo wakiwa wamebeba karatasi za mitihani katika shule mbalimbali waliona mwili wa mwanamume mmoja ukiwa umetupwa kando ya barabara ya Milima-Mitatu Radi.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Molo, Timon Odingo, mwanamume huyo alijulikana sana na wakazi kwa kuwa kiatu kimoja cha marehemu kilipatikana karibu na mwili huo.

Polisi walianzisha uchunguzi kubaini chanzo cha kifo cha mwanamume huyo.

  • Tags

You can share this post!

Karua: Washukiwa wengi wa ufisadi wanaoachiliwa ni wa...

Avril achanganya mashabiki kwa kumsamehe J Blessing...

T L