• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Wakazi wateketeza lori lililogonga na kuua mwanafunzi

Wakazi wateketeza lori lililogonga na kuua mwanafunzi

Na GERALD BWISA

WAKAZI wenye ghadhabu katika eneo la Likuyani, Kaunti ya Kakamega, Jumanne waliteketeza lori lililogonga na kuua mwanafunzi na kujeruhi vibaya baba yake.

Lori hilo liligonga Boniface Kakai, 43, alipokuwa akipeleka bintiye shuleni kwa kutumia baiskeli.

Kisa hicho kilitokea saa moja asubuhi katika eneo la Chemororoch kwenye barabara ya Kitale–Eldoret.

Mwanafunzi huyo, Cynthia Matasi, aliyekuwa akisoma katika Shule ya Msingi ya St Teresa, alifariki papo hapo.

Kamanda wa Polisi wa Uasin Gishu Ayub Ali alithibitisha mauaji hayo huku akisema kuwa lori hilo lenye nambari za usajili KCL 872S lilikuwa limebeba matofali na liliendeshwa na Joseph Gichuru Karanja, 38.

“Kakai alikuwa amebeba bintiye yake kwenye baiskeli akimpeleka shule kabla ya kukumbana na ajali hiyo. Kakai na lori wote walikuwa wakielea upande mmoja. Lori liligonga baiskeli kutoka nyuma,” akasema Bw Ali.

Kakai alikimbizwa katika Hospitali ya Matunda ambapo anaendelea kutibiwa.

Wahudumu wa bodaboda waliokuwa na ghadhabu walizuilia gari na kulichoma huku dereva akitoroka.

Maafisa wa polisi waliingilia kati na kutuliza vurugu.

Mwili umehifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya Rufaa ya Kitale.

You can share this post!

Laikipia yalipuka

KINA CHA FIKIRA: Wakati ni sasa, tumia leo kutengeneza...