• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
Wakili wa Serikali aagiza Miguna aruhusiwe kurudi

Wakili wa Serikali aagiza Miguna aruhusiwe kurudi

Na WANDERI KAMAU

WAKILI Mkuu wa Serikali, Bw Ken Ogeto, ameziagiza wizara za Mashauri ya Kigeni na Usalama wa Ndani kuhakikisha wakili Miguna Miguna amepata stakabadhi za usafiri kutoka kwa ubalozi wa Kenya nchini Canada na Ujerumani.

Kwenye barua aliyomwandikia wakili Nelson Havi, anayemwakilisha Dkt Miguna, Bw Ogeto aliziagiza wizara hizo kuhakikisha maafisa katika balozi hizo mbili wamezingatia maagizo ya mahakama, kwa kumpa wakili huyo stakabadhi anazohitaji ili kumwezesha kusafiri nchini.

Hatua hiyo ilifuatia barua ambayo Bw Havi alimwandikia Bw Ogeto, kumrai kuhakikisha idara husika zimezingatia agizo lililotolewa na Mahakama Kuu kumpa Dkt Miguna stakabadhi za usafiri anazohitaji.

“Tumepokea hakikisho kutoka kwa Wizara ya Usalama wa Ndani kwamba Idara ya Uhamiaji imewaagiza maafisa wake katika balozi za Kenya jijini Ottawa (Canada) na Berlin (Ujerumani) kumpa Dkt Miguna stakababadhi anazohitaji baada yake kujaza fomu maalum,” akasema Bw Ogeto.

Dkt Miguna alikuwa amepanga kurejea nchini mnamo Novemba 16, lakini safari yake ikasambaratika, baada ya Shirika la Ndege la Air France kusema limepokea agizo kutoka kwa serikali ya Kenya kutomruhusu kusafiri.

Baadaye, alidai “kuhangaishwa” na maafisa wa ubalozi wa Kenya nchini Ujerumani, alipowapelekea agizo la Mahakama Kuu kuwataka kumpa stakabadhi za usafiri.

Dkt Miguna amekuwa uhamishoni nchini Canada tangu 2018, baada ya kurejeshwa kwa nguvu na serikali kwa kumwapisha kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kama “rais wa wananchi.”

You can share this post!

Chebukati sasa akataa ‘kupangwa’

Uhuru asifia mchango wa jeshi kuinua uchumi

T L