• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Uhuru asifia mchango wa jeshi kuinua uchumi

Uhuru asifia mchango wa jeshi kuinua uchumi

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta, Jumanne alitetea hatua yake kuendelea kutumia Jeshi la Kenya (KDF) kusimania idara na miradi mbalimbali ya serikali, akisema limemsaidia pakubwa kutimiza ajenda zake za maendeleo.

Akitoa hotuba maalum kwa Bunge na Seneti kuhusu mafanikio ya serikali yake, Rais Kenyatta alitaja hatua hiyo kama iliyoleta mafanikio makubwa kwa miradi iliyoonekana kusambaratika kabisa.

Baadhi ya miradi aliyosifia kuboreshwa na jeshi ni Kiwanda cha Serikali cha Nyama (KMC), reli za Nairobi-Nanyuki, Nakuru-Kisumu na Bandari ya Kisumu.

Alisema kuwa kabla ya jeshi kuchukua usimamizi wa KMC, kiwanda kilikuwa kikipata faida ya Sh8,000 pekee kwa siku.

Hata hivyo, alisema baada ya jeshi kuanza kusimamia kiwanda hicho, kilianza kupata faida ya Sh1 milioni kila siku.

“Kitakwimu, mapato hayo yanamaanisha kuwa kiwanda hicho hupata faida ya Sh30 milioni kila mwezi na Sh3.6 bilioni kila mwaka. Yale tunayopaswa kujiuliza ni wapi zilikokuwa zikienda fedha zinazopatikana kwa sasa? Hili linatudhihirishia mafanikio makubwa yanayotokana na usimamizi mzuri wa wanajeshi wetu,” akasema.

Alisema kuwa kabla ya jeshi kuchukua usimamizi wa kiwanda hicho, wakulima na wafugaji walikuwa wakicheleweshewa malipo yao kwa hadi miaka minne, hali ambayo imebadilika, kwani kwa sasa huwa wanapokea malipo yao kwa muda wa siku tatu pekee.

Rais Kenyatta alisema kushiriki kwa jeshi kwenye ukarabati wa reli ya Nairobi-Nanyuki kumeboresha mapato ya wakulima na wafugaji, kwani imekuwa rahisi kusafirisha mifugo hadi katika masoko mbalimbali.

Alisema kuwa isingekuwa ni mchango wa jeshi kukarabati upya reli ya Nakuru-Kisumu, huenda mafanikio yanayoshuhudiwa kwa sasa hayangepatikana.

Kuhusu Bandari ya Kisumu, alisema ufufuzi wake umeboresha sana biashara kati ya Kenya na Uganda, hasa kwenye usafirishaji wa mafuta.

“Kabla ya ukarabati wa bandari hiyo, malori ya kusafirisha mafuta yalikuwa yakichukua hadi saa 72 ili kukaguliwa katika mpaka kati ya Kenya na Uganda. Hata hivyo, ufufuzi wa huduma za meli katika kiwanda hicho umeiwezesha Kenya kusafirisha karibu lita milioni nane za mafuta kila siku,” akasema.

Kauli yake inaonyesha huenda akakosa kubadilisha mtindo huo, licha ya kupata ukosoaji kutoka kwa baadhi ya mashirika ya kutetea haki za umma.

Baadhi ya idara ambazo zinasimamiwa na wanajeshi ni Halmashauri ya Kusimamia Jiji la Nairobi (NMS), Mamlaka ya Kununua na Kusambaza Dawa (KEMSA), Idara ya Magereza (KPS) kati ya nyingine.

You can share this post!

Wakili wa Serikali aagiza Miguna aruhusiwe kurudi

KRA kupiga mnada mizigo iliyoachwa

T L