• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Wakulima na wakazi wa Nyeri washerehekea mvua

Wakulima na wakazi wa Nyeri washerehekea mvua

KNA na WINNIE ONYANDO

WAKULIMA na wakazi wa Nyeri wanasherehekea baada ya kupokea mvua ya El Nino iliyotarajiwa kunyesha mwezi huu.

Kufuatia ripoti ambayo ilitolewa na Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa (KMD) mnamo Agosti mwaka huu, Mtaalamu wa Hali ya Hewa wiki jana aliwashauri wakulima kutarajia mvua kuanzia wiki hii.

Kwa mujibu wa ripoti, mvua za miezi ya Oktoba-Novemba-Desemba zilipaswa kuanza mwishoni mwa wiki ya pili na mwanzoni mwa wiki ya tatu ya mwezi huu.

Hata hivyo, baadhi ya maeneo hayajapokea mvua kama ilivyotabiriwa na hapo awali, jambo lililomfanya Mkurugenzi wa Huduma za Hali ya Hewa wa Kaunti Bw John Muiruri kufafanua kuwa mvua hiyo ilitarajiwa kuanzia wiki ya pili na ya tatu ya Oktoba.

“Unajua (mvua) inaweza kuchelewa kidogo. Kwa hivyo, nadhani sio mbali sana na muda uliotabiriwa,” Bw Muiruri aliambia KNA wiki jana.

Mary Wachira ni miongoni mwa wakulima ambao wamefurahia kuanza kwa mvua akisema ni ishara kuwa atapata mavuno.

Bi Wachira ambaye anaishi eneo la Gatitu katika Nyeri ya Kati anasema kuwa ana uhakika mvua hiyo ingeanza kunyesha wiki hii na tayari amelitayarisha shamba lake la ekari 10.

“Ninashukuru kwamba mvua sasa imeanza kunyesha kwetu tena baada ya kungoja kwa wiki nyingi. Ingawa sikupata fursa ya kusoma ripoti ya mtaalamu wa hali ya hewa, nilijua kutokana na uzoefu nilioupata katika safari yangu yote ya kilimo kwamba mvua itanyesha kuanzia Oktoba 19,” akasema Bi Wachira.

Kwa upande wake, Charles Chege, mkazi wa kijiji cha Gathuthi alisema mvua hiyo imekuwa afueni kubwa kwa familia yake kwani mahindi na maharagwe tayari yalikuwa yameota.

“Nina furaha kubwa sasa kwamba mvua imenyesha na pamoja na hakikisho kwamba tunaweza kupata mavuno baadaye mwaka ujao,” akaeleza Bw Chege.

KNA ilipomshinikiza Bw Muiruri kueleza iwapo mvua zinazoendelea kunyesha ni mvua zinazosubiriwa kwa hamu, alifafanua kuwa watu wanapaswa kutofautisha kati ya matukio ya El Nino na mvua wa kawaida.

Lakini hata kaunti inapofurahia kuanza kwa mvua, wakulima wanaoishi katika maeneo ya milimani wameonywa kuhusu uwezekano wa kupoteza mazao yao yote kutokana na mafuriko.

Hii inafuatia matukio sawia ambayo yameripotiwa Turkana na Kitui ambapo mvua inayoendelea kunyesha ikuathiri mimea.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi wa Liwale, Tanzania wadai uhaba wa maji unahatarisha...

Kwani unatumia simu ya ‘katululu’? DJ Mo azushia polisi...

T L