• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Wakazi wa Liwale, Tanzania wadai uhaba wa maji unahatarisha ndoa zao

Wakazi wa Liwale, Tanzania wadai uhaba wa maji unahatarisha ndoa zao

Na BAHATI MWATESA, Mwananchi Communications Limited

Wakazi zaidi ya 3,000 wanaoishi katika kijiji na Kata ya Kimambi, wilayani Liwale, wanaiomba Serikali kuwaongezea tanki lingine la maji kwani lililopo halikidhi mahitaji ya wakazi hao na maji yaliyopo sasa ni ya chumvi ambayo hayafai kwa matumizi ya kunywa.

Wakizungumza na Mwananchi Dijitali, wakazi hao wanasema kwamba wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita tano usiku wa manane kufuata maji na kuweka ndoa zao hatarini pamoja na uhai wao.

Wanasema kuwa maji wanayotumia sasa hivi wanapikia na kufulia kwa shida kwa sababu maji safi ambayo ni ya chemichemi yapo mbali na wanayapata kwa kulazimika kutembea umbali wa kilomita tano.

Hawa Shaweji ambaye ni mkazi wa kata ya Kimambi, anasema kuwa wanatembea kila siku katika eneo la Njengani na kwamba wakati wanakwenda kuchota maji wanakutana na wanyama wakali kama tembo ambao wanahatarisha maisha yao.

“Natoka nyumbani saa tisa usiku kwenda kuchota maji, kurudi tayari mchana. Hivi ni mwanamume gani anaweza kuvumilia hali hiyo, tunagombana na waume zetu kila wakati. Mimi naomba Serikali itupatie tanki kubwa lililo na maji salama kama yale ya chemichemi ili kutuondolea bughdha hii,” asema Hawa.

Mkazi mwingine, Mussa Litago anasema kuwa maji wanayoyapata katika chemichemi hiyo ni foleni ndefu akisema wanaweza kwenda asubuhi wakarudi jioni. Wanakwenda umbali mrefu kwa kuwa wanahitaji maji ya kunywa ambayo hayana chumvi.

“Tunakwenda umbali mrefu kwa kuwa maji ni baridi na yanatusaidia kwa kunywa, maji yaliyopo sasa ambayo tumewekewa tanki dogo ni ya chumvi. Haya maji ya chumvi tunayatumia kwa ajili ya kufulia, kupikia na kuoshea vyombo. Sisi wananchi wa Kimambi tunateseka sana maji, Serikali isaidie kuleta maji safi na salama,” asema Litago.

Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) wilayani Liwale, Mhandisi Joseph Mbio anasema kuwa katika kata hiyo wanacho chanzo kimoja ambacho ni kisima na wamewekewa tanki, changamoto iliyopo ni kwamba maji hayo ni ya chumvi. Anasema wameshaongea na watu wa Bonde la Mto Ruvuma kwa ajili ya kufanya utafiti ili kuweza kuchimba kisima kingine ili wapate maji safi ambayo siyo ya chumvi.

“Ruwasa tumeshaongea na watu wa Mto Ruvuma kuja kufanya utafiti ili kuweza kuchimba kisima kingine ili wananchi waweze kupata maji yaliyo safi zaidi ambayo yatakuwa hayana chumvi,” anasema Bw Mbio.

  • Tags

You can share this post!

Maji yamkaribia Trump shingoni mshirika wake wa pili...

Wakulima na wakazi wa Nyeri washerehekea mvua

T L