• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Wakulima wa viazi vitamu walalamikia bei duni

Wakulima wa viazi vitamu walalamikia bei duni

Na KENYA NEWS AGENCY

WAKULIMA wa viazi vitamu kutoka Kaunti ya Elgeyo Marakwet wamelalamikia bei ya chini ya zao hilo huku wakiwakashifu mabroka kwa kuchangia kushuka kwa bei hizo na kuwatumbukiza kwenye umaskini.

Ikizingatiwa huu ni msimu wa mavuno, wakulima hao wanadai kuwa mawakala wamekuwa wakikita kambi katika mashamba yao ili kuwashawishi wauze viazi vyao na pia kuwaamulia bei.

Mkulima Hillary Kimutai kutoka Kapyego alisema kuwa wamekuwa wakitegemea kilimo cha viazi vitamu kupata hela japo bei ya kila gunia ya kilo 50 imepungua kutoka Sh2,000 hadi Sh500 kwa muda wa mwezi moja uliopita.

“Tumekuwa tukipata hasara kubwa kwa sababu mabroka wananunua viazi vyetu kwa bei ya chini kisha kuviuza sokoni kwa bei ya juu. Kama wakulima tumeshawishika kuingia kwenye mtego wao kwa sababu serikali ya kaunti haina utaratibu maalum wa kuvinunua,” akasema Bw Kimutai.

Pia, Bw Kimutai alisema kuwa mji wa Eldoret ambao ni soko lao kubwa ni mbali kutoka mashamba yao huku wakulima wengi wakikosa mbinu na jinsi ya kumudu gharama ya kusafirisha viazi hivyo sokoni.

Aidha, kafyu iliyowekwa katika kaunti za Magharibi na Nyanza ambazo ni soko la kuuzia viazi hivyo, iliathiri mauzo hayo japo wanatarajia sasa hali iimarike baada ya kuondolewa wiki jana.

Hata hivyo, Waziri wa Biashara wa kaunti hiyo Anne Kibosia aliwashauri wakulima wawakatae mabroka hao na badala yake waunde vyama vya ushirika ndipo kaunti iwe katika nafasi nzuri ya kuwasaidia kupata soko la mazao yao.

Pia aliwataka wakulima wazamie kilimo cha ufugaji na kile cha mimea mingine badala ya viazi pekee ambako mabroka wamekuwa wakiwafilisi na kujitajirisha.

You can share this post!

Wapwani wakaushwa tena

Mzozo wa nyadhifa ODM watishia kuangusha chama