• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 12:52 PM
Waliofanya kazi ya IEBC kusubiri zaidi malipo yao ya Sh1.9bn

Waliofanya kazi ya IEBC kusubiri zaidi malipo yao ya Sh1.9bn

NA MARY WANGARI

WAKENYA waliotoa huduma zao na bidhaa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika uchaguzi mkuu uliopita na chaguzi ndogo zilizofuatia nchini watalazimika kusubiri hata zaidi kabla ya kupokea malipo yao.

Karibu miezi minane imepita tangu uchaguzi mkuu ulipofanyika mwaka 2022, IEBC ingali haijalipa jumla ya Sh1.949 bilioni kwa maafisa wa IEBC na wafanyabiashara kwa kazi waliofanya wakati wa uchaguzi uliofanyika katika kaunti zote 47.

Miongoni mwa fedha hizo, Kaunti ya Bungoma inaoongoza kwa jumla ya Sh264 milioni zinazojumuisha Sh119.6 milioni zinazodaiwa na maafisa wa uchaguzi huku wafanyabiashara wakidai Sh144.2 milioni kwa bidhaa na huduma zilizotumika katika uchaguzi mkuu na chaguzi ndogo za useneta zilizofuatia.

Katika eneobunge la Kabuchai maafisa wa uchaguzi na mashirika wangali wanasubiri malipo yao ya jumla ya Sh19.9 milioni kwa kazi waliofanya katika uchaguzi huo mkuu na chaguzi ndogo zilizofuatia, Bunge lilielezwa jana.

Pesa hizi zinajumuisha Sh1.09 bilioni pamoja na Sh900 milioni zinazodaiwa na maafisa wa IEBC na mashirika ya bidhaa na huduma mtawalia, Naibu Mkurugenzi wa IEBC, Obadiah Keituny alisema alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Sheria na Masuala ya Haki.

Bw Keituny alifichua kuwa baadhi ya maafisa wa IEBC Bungoma wamegoma kwenda kazini baada ya kusubiri malipo hayo kwa muda mrefu bila mafanikio.

Alisema licha ya kuitisha mara kadhaa Sh4.4 bilioni kutoka kwa serikali ili kuwalipa maafisa wa IEBC na mashirika hayo ya bidhaa na huduma, tume hiyo haijafanikiwa huku akiomba Bunge kuingilia kati.

“Tume imeanza kutoa malipo kwa mashirika mbalimbali ya bidhaa na huduma waliohusika katika uchaguzi mkuu na chaguzi ndogo zilizopita. Kufikia Aprili 4,2023, Tume ilikuwa imeitisha jumla ya Sh4.4 bilioni kutoka kwa Hazina Kuu. Pesa hizi zinajumuisha kiasi cha Sh1.9 bilioni kilichoitishwa katika tarehe mbalimbali tangu Oktoba 3, 2022 ili kuwalipa wauzaji bidhaa na watoaji huduma katika kaunti zote,” ilisema taarifa iliyowasilishwa na IEBC.

“Kutokana na yanayoendelea, pesa zilizosalia zitalipwa zitakapotolewa na Hazina Kuu. Kwa hivyo tunaomba Kamati iingilie kati.” Kulingana na afisa huyo, endapo pesa hizo hazitatolewa katika bajeti ya mwaka huu, pesa hizo zitarejeshwa kutoka kwenye mfumo wa malipo, hivyo basi kuongeza kiwango cha madeni ambayo hayajalipwa.

“Jambo hili huenda likasababisha ada za ziada kama vile riba na ada za kesi kutokana na ucheleweshaji wa malipo. Wafanyabiashara walioathirika huenda wakakataa kutoa huduma muhimu kutokana na malipo yao kucheleweshwa,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Wito Kenya Power itumie tariff maalum kwa kampuni za maji

Ramadhani yazidi kunoga mji na mitaa hailali usiku

T L