• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Waliopatikana na pombe kituo cha polisi wachekesha korti

Waliopatikana na pombe kituo cha polisi wachekesha korti

Na RICHARD MUNGUTI

WANAUME wawili walifanya kila mmoja katika mahakama moja ya Nairobi kuangua kicheko walipoungama “tulikutwa na Muratina (pombe ya kienyeji) ndani ya kituo cha polisi cha Kabete ya kusherehekea kufufuka kwa Mwokozi Yesu Kristo alipomshinda Ibilisi msalabani.”

Mabw Joseph Kirui na Shadrack Tanui waliungama hayo waliposhtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Kibera Bi Esther Boke kwa kupatikana na lita mbili ya Muratina.

Kirui na Tanui walikiri makosa dhidi yao na kuapa kueleza korti ukweli.

Wakijitetea walisema, “ Ukweli ni kwamba tulipatikana na pombe hii haramu ndani ya kituo cha Polisi cha Kabete. Tulikuwa tumeenda kumlipia dhamana rafiki yetu aliyekuwa amekamatwa. Hii ndio nambari ya OB ( occurrence book number) ya mwenzetu huyo.”

Bw Tanui alieleza korti kuwa walikuwa wameweka Muratina hiyo ndani ya gari lao nambari ya usajili KCL 819R.

“Polisi walitufuata na kuona hii Muratina ndani ya gari letu ndipo wakatugeuka na kutushika kisha wakatufungulia shtaka la kupatikana na pombe haramu,” alisema bw Tanui akijitetea.

Mshtakiwa huyo aliomba mahakama msamaha akisema , “Haki mheshimiwa hata kama niko na wazimu nitabugia Muratina ndani ya kituo cha Polisi?”

Bw Tanui alisema Muratina hiyo walikuwa wamebarikiwa nayo na rafiki yao “washerehekee kufufuka kwa Yesu.Tena hii lita mbili itatutosha sisi wanaume wenye matumbo saizi hii (huku akishika tumbo lake).”

Aliomba korti iwasamehe na kuapa kutoenda ndani ya kituo cha polisi siku nyingine wakiwa na kileo.

“Tumegundua polisi hawana rafiki.Tulienda kumwokoa mwenzetu kumbe tumejipeleka kwa mdomo wa Simba,” akarai Bw Tanui.

Hakimu aliwasamehe na kuwaachilia huru.

Baada ya kusamehewa , wawili hao waliinama mbele ya mahakama ya Kibera na kusema kwa sauti ya juu , “ Haki Mungu akubaribi Bi hakimu.”

Wawili hao waliondoka kizimbani aste aste huku. Bi Boke aliamuru pombe hiyo iahiribiwe mara moja.

  • Tags

You can share this post!

TANZIA: Mume wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza afariki

Mwanaharakati taabani kwa kutania Rais