• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Wanafunzi 500 Landi Mawe wapokea basari, wahimizwa watie bidii masomoni

Wanafunzi 500 Landi Mawe wapokea basari, wahimizwa watie bidii masomoni

NA SAMMY KIMATU

WANAFUNZI zaidi ya 500 kutoka familia maskini katika wadi ya Landi Mawe, eneobunge la Starehe wamepigwa jeki kielimu baada ya kupokea basari.

Akiongea kwa niaba ya Bw Simon Maina ‘Miche Miche” aliye mwakilishi bunge wa wadi hiyo, Bw Stephen Okwach Isa ambaye ni Msaidizi wa Bw Maina ameambia Taifa Leo baadhi ya walionufaika ni wale waliokosa basari muhula uliopita.

Bw Isa aliongeza kwamba changamoto kuu katika wadi hiyo ni kwamba walio na hitaji ya basari ni wengi kuliko mgao wanaopokea kutoka kwa serikali ya kaunti ya Nairobi.

“Landi Mawe ina mitaa kadhaa ya mabanda ambako watoto kutoka familia zinazohitaji kusaidiwa zinapiku kiasi cha hela tunazopewa na serikali kukidhi hitaji ya basari,” ujumbe wa Bw Maina uliandikwa na kusomwa na Bw Isa.

Aidha, miongoni mwa waliofaidika na basari hizo ni wanafunzi wanaosomea katika shule za upili, waliojiunga kwenye taasisi za kiufundi na kundi la vijana 20 wanaosomea udereva,” Bw Maina akasema kwenye hotuba huyo iliyoandikwa.

Katika basari za muhula huu, waliopokea hundi za Sh5,000 kila mmoja walikuwa ni watu 540.

Bw Maina alisema idadi hiyo ilishuka ikilinganishwa na watu 600 waliofaidika na basari kwenye awamu ya kwanza ambapo basari zilisambazwa kwa wakazi wa Landi Mawe muhula wa kwanza.

Vilevile, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za kiongozi huyo katika Jumba la Garage eneo la Commercial, Bw Maina pia aliwasambazia chakula cha msaada.

Tofauti na misaada iliyopeanwa hapo awali kama ilivyo ada ya misaada kutoka kwa wanasiasa, Bw Maina aligawia wakazi chakula tofauti.

Chakula hicho kilikuwa ni mseto wa pakiti ya Unga wa mahindi na pakiti ya unga wa ngano.

Isitoshe, aligawa Sukari na mafuta ya kupikia kwa waliokuwa kwenye hafla hiyo.

Kadhalika, Bw Maina aliwashauri viongozi kuweka tofauti zao za kisiasa na kuangazia nchi ya Kenya na Wakenya akirejelea maandamano ya Jumatano.

“Ni muhimu kuwa na kikao cha mazungumzo kwa mirengo yote miwili kwa manufaa ya Kenya na Wakenya iwe ni upande wa Kenya Kwanza au Azimio la Umoja One Kenya Alliance,” Bw Maina akashauri.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Serikali ya Kenya Kwanza yapata asilimia 30.8 pekee kwa...

UFAA yashauri Wakenya kufuatilia mali zao zisipotee

T L