• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 3:09 PM
Serikali ya Kenya Kwanza yapata asilimia 30.8 pekee kwa uchapakazi – Utafiti

Serikali ya Kenya Kwanza yapata asilimia 30.8 pekee kwa uchapakazi – Utafiti

STEVE OTIENO Na WINNIE ONYANDO

UTAFITI wa Trends and Insights For Africa (TIFA) unaonyesha Wakenya wanaipa serikali ya Kenya Kwanza asilimia 30.8 pekee kwa uchapakazi.

Aidha, asilimia 56 ya Wakenya wanahisi Kenya inachukua mkondo mbaya. Hii ni kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha, suala ambalo Rais Ruto aliahidi kushughulikia ndani ya siku 100 mamlakani.

Hivyo ni wazi kwamba asilimia kubwa ya Wakenya wanaamini Rais William Ruto hajafaulu kutimiza ahadi alizotoa tangu achaguliwe mnamo Agosti 9, 2022.

Utafiti huo ulifanyika kati ya Juni 24 na 30, 2023.

Utafiti unaonyesha ni wazi kuwa Rais hajaweza kutimiza ahadi hiyo huku bei ya bidhaa muhimu kama vile unga, mafuta ya kupikia na sukari ikiendelea kupanda.

Utafiti umebainisha kuwa asilimia 56 ya Wakenya wanaamini kuwa Kenya inaelekea pabaya kutokana na hali ngumu ya maisha. Utafiti wa awali uliofanywa na TIFA mwezi Machi ulionyesha kuwa asilimia 37 ya Wakenya waliamini kuwa nchi inaelekea pazuri lakini idadi hiyo ilipungua hadi asilimia 25 mwezi Juni.

“Bila kujali itikadi zao za kisiasa, idadi kubwa ya Wakenya wanaamini kuwa nchi inaelekea pabaya. Hii ni kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha,” ripoti hiyo ilisema.

Angalau Wakenya watano kati ya kumi (asilimia 52) wanaamini serikali ya Kenya Kwanza imeshindwa kudhibiti kupanda kwa gharama ya maisha.

“Idadi ya watu wanaoamini kuwa serikali ya Kenya Kwanza imeshindwa kushughulikia suala la kupanda kwa gharama ya maisha inazidi kuongezeka.”

Sababu nyingine za kuamini kuwa nchi inaelekea pabaya ni Sheria ya Fedha 2023 ambayo itawalazimisha Wakenya kulipa ushuru wa ziada.

“Asilimia tatu ya Wakenya wanaamini kuwa hatua ya serikali ya kuongeza ushuru sio njema. Kadhalika, asilimia moja wanaamini nchi inaelekea pabaya kutokana na uongozi mbaya, uteuzi wa serikali (asilimia moja), kuongezeka kwa ukosefu wa usalama katika North Rift (asilimia moja) na kuongezeka kwa deni la umma (asilimia moja),” ripoti hiyo ilisema.

Ingawa mradi wa Hustler Fund, uliozinduliwa na Rais Ruto muda mfupi baada ya kuapishwa Septemba 2022, uliorodheshwa kama mafanikio muhimu ya utawala wa sasa na asilimia 29 ya Wakenya, umaarufu wake kufikia Juni, 2023 ulipungua hadi asilimia 10.

Hata hivyo Wakenya wanaoamini serikali inaelekea pazuri wametaja sera ya ulipaji wa deni (asilimia nne), kuajiri walimu zaidi (asilimia tatu), kukamilisha na kuzindua miundombinu (asilimia tatu) pamoja na kutoa ajira na usaidizi wa kifedha kwa wahitaji (asilimia mbili) kuwa miongoni mwa sera zinazoonyesha tunaelekea pazuri kama nchi.

Zaidi ya theluthi moja ya Wakenya (asilimia 34) wanaamini kuwa Waziri wa Usalama Profesa Kithure Kindiki ndiye waziri anayetekeleza majukumu yake kikamilifu. Anayemfuatia Profesa Kindiki ni Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu kwa asilimia saba.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge Patrick Makau aachiliwa baada ya kuhojiwa na DCI...

Wanafunzi 500 Landi Mawe wapokea basari, wahimizwa watie...

T L