• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
UFAA yashauri Wakenya kufuatilia mali zao zisipotee

UFAA yashauri Wakenya kufuatilia mali zao zisipotee

NA LAWRENCE ONGARO

MAMLAKA ya kuhifadhi fedha na mali za umma zisizodaiwa, Unclaimed Financial Assets Authority – UFAA), imetoa wito kwa Wakenya kudai fedha hizo.

Mkurugenzi wake Bw John Mwangi, alisema ni watu wengi sana walio na mali zao katika mashirika mengi na hawajazichukua.

Alisema UFAA inahifadhi fedha za watu walio hai na pia waliofariki.

Alisema kuna takribani jumla ya Sh57 bilioni wanazohifadhi na ambazo wanaona ni vyema zikiwafikia wenyewe.

“Iwapo una jamaa yako popote pale aliyefariki na ungetaka kufuatilia mali yake, unaweza kufika katika ofisi zetu zilizoko kwenye kaunti,” alisema Bw Mwangi.

Alisema shughuli hiyo inaendeshwa kwa ushirikiano na ofisi za Huduma Centre.

Aliwahimiza wananchi popote walipo wachukue nafasi hiyo kufuatilia mali zao ili zisipotee bure.

Alisema kwa muda wa miezi michache tu wamerejesha takribani Sh2 bilioni kwa wanaostahili kuzipokea.

“Tunaelewa hali ya uchumi ni ngumu wakati huu kwa hivyo fedha hizo ni muhimu kwa wenyewe,” alisema Bw Mwangi.

Naye Mwenyekiti wa UFAA Dkt Francis Kigo, alisema ni mchakato unaochukua muda wa siku 10 pekee kabla ya mtu kupokea fedha zake zilizokwama.

“Tunawahimiza wananchi popote walipo wachukue nafasi hiyo kufuatilia mali zao ambazo imewachukua muda mrefu pengine wakizifuatilia,” alieleza Dkt Kigo.

Mkurugenzi wa Huduma Centre Bw Ben Chilumi alisema wakishirikiana na UFAA kuhudumia wananchi, tayari wamezuru maeneo matatu hivi karibuni na ambayo ni Nakuru, Nyeri na Thika.

“Tutafanya juhudi kuzuru kaunti zote nchini,” alisema Bw Chilumi.

Bw Samuel Kamau ambaye alifika kufuatilia fedha za mkewe zilizokuwa kwa simu, alipata hakikisho ya kulipwa fedha hizo chini ya siku 10 zijazo.

Alipongeza mpango huo akisema utasaidia wananchi pakubwa.

“Ninahimiza raia wenzangu wajitokeze kwa wingi ili kufuatilia mali zao zilizokosekana kutambuliko ziliko kwa sababu moja au nyingine,” alisema Bw Kamau.

  • Tags

You can share this post!

Wanafunzi 500 Landi Mawe wapokea basari, wahimizwa watie...

Rais Raisi ashambulia nchi zinazolazimisha Uganda...

T L