• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Wanafunzi wa vyuo vikuu kushiriki katika mashindano yanayolenga kuboresha ujuzi katika sekta ya ujenzi

Wanafunzi wa vyuo vikuu kushiriki katika mashindano yanayolenga kuboresha ujuzi katika sekta ya ujenzi

NA WINNIE ONYANDO

ZAIDI ya wanafunzi 30 kutoka vyuo vikuu vitano mashuhuri nchini wanatazamiwa kushiriki katika mashindano ya kila mwaka yanayofadhiliwa na kampuni ya Mabati Rolling Mills ikishirikiana na Muungano wa Wasimamizi wa Ujenzi Nchini (ACMK).

Mashindano hayo yanalenga kuimarisha ujuzi wa wanafunzi na kuwawezesha kutumia mafunzo ya darasani nyanjani.

Uzinduzi wa toleo hilo la nne la mashindano ulifanyika Jumatano katika shirika la MRM jijini Nairobi na kuwaleta pamoja wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi (UON), Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT), Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU), Chuo cha Kiufundi cha TUM na Chuo Kikuu cha Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST).

Mashindano hayo yanalenga kuimarisha sekta ya ujenzi ili nchi iwe na watu walio na ujuzi hitajika.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa hafla hiyo, Meneja wa Masoko MRM Rittah Okello alisema kuwa wanafuraha kuendeleza ushirikiano wao na ACMK katika mpango huo.

“Tunaamini kuwa mashindano hayo yatasaidia katika kuimarisha sekta ya ujenzi,” akasema Bi Okello.

Bi Okello alifichua kuwa shindano hilo lilizinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2018, huku shindano la kwanza likifanyika 2019.

Rittah Okello akiwa na baadhi ya wanafunzi wanaotarajiwa kushiriki mashindano ya kila mwaka yanayofadhiliwa na kampuni ya Mabati Rolling Mills (MRM) ikishirikiana na Muungano wa Wasimamizi wa Ujenzi Nchini (ACMK). PICHA | WINNIE ONYANDO

Naye Ilbert Abiri, Mwenyekiti wa ACMK, alitoa shukrani kwa ushirikiano unaoendelea na MRM, akisisitiza kuwa shindano hilo linawapa wanafunzi jukwaa la kipekee la kuweka kwenye matendo yale waliyofunzwa shuleni.

Shindano hili linawakilisha hatua kubwa katika kuboresha uzoefu wa kielimu wa wanafunzi wa usimamizi wa ujenzi huku likikuza ushirikiano kati ya wasomi na sekta ya ujenzi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ushiriki wa Wanafunzi, James Mburu, alisema kwa sasa vikundi 10 vimetuma ombi la kushiriki katika mashindano hayo huku kila kundi likiwa na wanafunzi kati ya watatu na wanne.

Kikundi kitakachoshinda kitazawadiwa Sh30,000 huku kikundi cha pili kikipokea Sh20,000 na cha tatu Sh15,000.

  • Tags

You can share this post!

Mazishi ya shujaa Muthoni Kirima kusubiri Gachagua...

AMINI USIAMINI: Samaki anayewinda kwa kutema maji kama...

T L