• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Wanajeshi na wahudumu wa afya Nakuru kuchanjwa

Wanajeshi na wahudumu wa afya Nakuru kuchanjwa

RICHARD MAOSI NA ERICK MATARA

WAHUDUMU wa afya katika Hospitali ya Rufaa ya Nakuru(PGH), ni miongoni mwa watu wa kwanza kupokea chanzo,ya kuwakinga dhidi ya msambao wa covid-19.

Zaidi ya wahudumu wa afya 11,000 kutoka kaunti ya Nakuru kuanzia madereva , walinzi, safu ya kupokea wagonjwa na wafanyikazi wengine watanufaika.

Operesheni hiyo ambayo ilianza rasmi siku ya Jumatatu, inalenga kufaidi Kaunti nyinginezo kama vile Baringo, Narok, Bomet, Samburu na Kericho.

Kulingana na Mkurugenzi wa Maswala ya Afya kutoka Nakuru, Bw Gichuki Kariuki usambazaji wa chanjo utaelekezwa kwa Hospitali zinazopatikana mashinani baadae.

“Katika Bonde la Ufa tulipokea chanjo 30,000 ya Astra Zeneca na tunalenga wahudumu wa afya katika chanjo hiyo ambayo itaendeshwa kwa awamu tatu.Ikumbukwe kuwa wakongwe ni miongoni mwa kundi muhimu la watu ambao watapokea chanjo katika awamu ya kwanza na ile ya pili,”akasema.

Aidha jumla ya chanjo 3000 zinatarajiwa kufika kwenye Kambi cha Wanajeshi cha Lanet Military Academy(KMA).

Gichuki aliambia Taifa Leo kuwa awamu ya kwanza, itakuwa kwa wahudumu wa afya wanaovalia sare na inatarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa Juni 2021.

Vilevile baina ya Julai 2021 na Juni 2022, wakongwe wenye zaidi ya miaka 50 na wale ambao wamepitiza miaka 18 watakuwa wamepokea chanjo.

Kaunti ya Nakuru ilipokea chanjo ya AstraZeneca wiki iliyopita.

Gichuki aliwaomba wakazi wa Nakuru , waendelee kujikinga dhidi ya msambao wa homa ya covid -19 hata baada ya kupokea chanjo.

“Ingawa hii tiba imekuja wakati muhimu kutukinga, cha msingi ni kila raia kuchukua wajibu wa kujikinga dhidi ya corona, kwa kuvalia maski, kunawa mikono na kudumisha umbali wa mita moja,”

Baadhi ya watu wa kwanza kupokea chanjo ni pamoja na Mkurugenzi mkuu wa Afya Bw Daniel Waweru,Benedict Osore na Elizabeth Kiptoo miongoni mwa wahudumu wengine.

You can share this post!

Simanzi mwanamuziki Kiambukuta akifa

Wananyuki wawika baada ya kuwanyuka wapinzani wao wa jadi...