• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Wanavyuo kupokea ufadhili wa wa Sh4.5 milioni kutoka kwa mfuko wa NG-CDF Thika

Wanavyuo kupokea ufadhili wa wa Sh4.5 milioni kutoka kwa mfuko wa NG-CDF Thika

Na LAWRENCE ONGARO

WANAFUNZI wa vyuo mbalimbali kutoka Thika, wamehimizwa kujiunga kwa vikundi ili wanufaike na fedha za maendeleo za NG-CDF.

Walishauriwa kuwa wabunifu katika kozi wanazofanya vyuoni ili baadaye wanapokamilisha masomo yao waanze kujitegemea kwa kujiajiri wenyewe.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema tayari Sh4.5 milioni zimetengwa ili kuwapa wanafunzi waliojipanga kujiendeleza kwa kazi fulani.

Aliwashauri wanafunzi wanaokamilisha masomo vyuoni kuwa na maono ili wawe waajiri mara watakapokuwa wamejiimarisha kwenye biashara zao.

“Iwapo wanafunzi watatumia vyema ujuzi wao bila shaka hawataweza kupata shida wanapokamilisha masomo yao,” aliwashauri Bw Wainaina.

Aliyasema hayo mjini Thika mnamo Jumamosi katika hafla ya wanafunzi ya maonyesho ya bidhaa tofauti wanazotengeneza na kuzitumia wakiwa vyuoni.

Zaidi ya vyuo 10 vilishiriki kwenye hafla hiyo iliyofana sana.

Mbunge wa Thika Patrick ‘Jungle’ Wainaina akiwa na baadhi ya wanavyuo katika hafla ya Juni 5, 2021. Picha/ Lawrence Ongaro

Mratibu wa hafla hiyo Bi Felista Wairimu alisema ilikuwa ya kufana kwa sababu vyuo kadha vilishiriki na kuonyesha ujuzi wao wa kutengeneza bidhaa tofauti na jinsi ambavyo zinatumika.

Baadhi ya vyuo vilivyohudhuria hafla hiyo ni Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU), Zetech, Cascades, Kenya Institute of Management (KIM), na Kenya Business and Counseling miongoni mwa vingine.

Baadhi ya kozi zinazoendeshwa kwenye vyuo hivyo ni uokaji wa keki, ushonaji wa nguo, ususi, ujenzi, masomo ya umeme, na mengine mengi.

Bi Wairimu alieleza kuwa wana mipango ya kuleta hafla nyingine za shule za chekechea, za msingi na hata wataalika viwanda tofauti vya Thika vije kuonyesha bidhaa.

“Tunataka washika dau wote wasiachwe nyuma bali wajitokeze na bidhaa zao ili zitambulike na wananchi,” alieleza Bi Wairimu.

Wanafunzi wengi waliridhika na mawaidha waliopokea kutoka kwa washika dau wote waliohudhuria hafla hiyo wakisema watajiunga kwa vikundi ili wanufaike na fedha za maendeleo za NG-CDF.

You can share this post!

Uswidi wapepeta Armenia 3-1 kirafiki

Mpango wa Tottenham kumwajiri kocha Antonio Conte watibuka